Ibara 39 (g): Kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam
Katika kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, jitihada za kujenga barabara mpya kwa kiwango cha lami, changarawe pamoja na kukarabati barabara zilizoharibika zinaendelea Pia kuna jitihada mbalimbali zilizofanywa na wadau kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam (TANROADS, TARURA, DMDP na DART), Mashirika ya Reli (TRC na TAZARA), kwenye uendeshaji wa vivuko (TEMESA), pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).
Miradi iliyotekelezwa na TANROADS
Kuna ongezeko la km 32.5 zilizojengwa kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kupunguza msongamano, ambapo barabara zilizojengwa ni zifuatazo; Korogwe - Maji Chumvi (km. 3.5 kwa gharama ya Tsh milioni 7,777), Kigogo – Dampo (km. 1.6 kwa gharama ya Tsh milioni 2,698), Kimara Baruti - Chuo Kikuu (km. 2.6 kwa gharama ya Tsh milioni 5,724), Goba – Mbezi (km. 7 kwa gharama ya Tsh milioni 14,230), Kifuru – Mbezi (km. 4 kwa gharama ya Tsh milioni 9,960) na Goba - Samaki Wabichi (km. 9 kwa gharama ya Tsh milioni 16,436) pamoja Goba – Madale (km. 5 kwa gharama ya Tsh milioni 9,950) ambapo ujenzi umekamilika kwa wastani wa asilimia 50%. Mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa flyover ya TAZARA km 1.4 ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2018 pamoja na ujenzi wa Interchange ya Ubungo ambapo Ujenzi huo unaendelea na upo katika hatua za awali na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2020, barabara ya njia sita; DSM- Chalinze km.128, Salender Bridge bypass km 6.8 ambapo upembuzi yakinifu umekamilika pamoja na Outer Ring Road inayounganisha Korogwe - Chanika na Bunju km 33. Pia ujenzi wa BRT phase II na III, zabuni zimetangazwa na taratibu za kumpata Mkandarasi zipo katika hatua za mwisho na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Disemba, 2018. Gharama ya miradi yote ni Tsh 158,526,000,550/=
Uzinduzi wa Daraja la Kigamboni (Nyerere)
Daraja la Nyerere lilizinduliwa rasmi na Mhe John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Daraja hili pamoja na barabara za maingilio lilijengwa na Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Mfuko wa Jamii (NSSF) kwa gharama Tsh bilioni 216 ambapo Serikali imetoa 40% na NSSF imetoa 60%. Barabara za maingilio kwa upande wa Kurasini yenye urefu wa km 2.5 zilikwisha kukamilika na kwa sasa wanaendelea na kipande cha Kigamboni kinachounganisha na barabara inayotoka Kigamboni kwenda Kibada.
Miradi iliyotekelezwa na TARURA
Ibara 39 (a) (iii) Kuanzisha Wakala/Taasisi itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Miji na Majiji na Halmashauri ambazo ziko chini ya TAMISEMI.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) ilianzishwa ili kuhudumia barabara zote zilizokuwa zinahudumiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Tangu walipoanza rasmi hadi Juni, 2018 wametumia kiasi cha Tsh. 31,184,703,230 /= kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya zaidi ya km 50 kwa kiwango cha lami na changarawe na matengenezo ya baadhi ya barabara zilizoharibika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Miradi iliyotekelezwa na DMDP
Uboreshaji wa Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano kupitia DMDP miradi iliyotekelezwa ni kama ifuatavyo:
Halmashauri ya Manispaa Temeke:
Ujenzi wa daraja 1 katika eneo la Kijichi – Toangoma, Madaraja 5 ya Nzasa - Kilungule – Buza. Ujenzi wa barabara zenye urefu wa km. 15.52 upo katika hatua za mwisho za kuweka alama za barabarani na barabara zenye urefu wa km.139.30 ambazo hatua mbalimbali za utekelezaji zinaendelea.
Mifereji ya maji ya mvua km. 40.82, katika maeneo ya Keko, Mpogo, Kijichi, Serengeti, Mtoni, Kilakala, Yombo Vituka, Makangarawe, Mbagala na Temeke, kalavati za boksi 9 na pipe kalvati 8, Ujenzi wa masoko mawili na vituo maeneo ya Mbagala na Kijichi, ujenzi wa masoko 7 katika maeneo ya Kiwalani (3), Mbagala kuu (1), Mtoni (1), Makangarawe (1) na Kilakala (1).Ujenzi wa kiwanja cha mpira eneo la Makangarawe na kituo cha Afya katika kata ya Buza utekelezaji wake unaendelea.
Kiasi cha Sh. 126,957,711,964 kinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa miradi hiyo.
Halmashauri ya Manispaa Kinondoni:
Ujenzi wa Barabara 21.68km za Makanya, Tandale-Kisiwani, Kilimani, Simu 2000, Kilongawima na CBD Makumbusho, External, Kisukuru, Korogwe-Kilungule na Maji ya Chumvi-Kilungule kwa kiwango cha Lami na Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami, Mifereji, Taa za Brarabarani, Njia za watembea kwa miguu na Vyoo vya Umma katika Kata ya Tandale, Mburahati na Mwananyamala na Ujenzi wa 10.2 Km Mto Sinza na Kiboko kuimarisha mifumo ya maji ya mvua upo katika hatua za mwanzo utekelezaji
Ujenzi wa Barabara za Shekilango kwa njia nne, TRA, Igesa, Mori na Mabatini (7.54km) pamoja na za Akachube (1km) na Makumbusho - Mwanamboka (5.42km) kwa kiwango cha Lami. Barabara hizi zinaunganishwa na barabara za mabasi ya mwendokasi ambapo ya Akachube inaunganishwa pia na Hopitali ya Rufaa ya Mwananyamala. Kazi ipo katika hatua za mapitio ya usanifu.
Kiasi cha Sh. 219,651,627,339 kinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa miradi hiyo.
Halmashauri ya Manispaa Ilala:
Ujenzi wa barabara za Mlisho 3.2 km za Ndanda, Kiungani, Omari Londo, Olympio, Mbarouk, Kongo, Livingstone, Swahili na Nyamwezi, Ujenzi wa mifereji ya chini, Ujenzi Ofisi na maabara kuweka taa za barabarani.
Ujenzi wa barabara kwenye makazi ya yasiyopangwa: Gongo la Mboto 7.77km za Chung’e, Kampala, Limbanga, High Mount na Baghdad pamoja na Ujenzi wa mtaro wa Gongo la Mboto 1.85km, Vizimba 7 vya taka, kununua gari 1 la kusomba taka. Kiwalani 10.35km barabara za Bush, Gude, Jongo, Mbilinyi, pepsi, Jamaka, zahanati, Kamungu, Mkwajuni, Binti Musa na Betheli. Kujenga vituo 3 huduma za vyoo, Vizimba 8, kununua gari 1 la kusomba taka, kujenga masoko 3, kujenga maeneo ya mapumziko 2, kujenga vituo 3 vya huduma za maji safi. Ukonga 12.29km barabara za Markaz, Zimbili, Dispensary, School na Chacha pamoja na kujenga Vituo 7 huduma za maji safi, Vizimba 9 vya taka.
Ujenzi wa mifereji mikubwa 15.96km ya Mafuriko, Buguruni Kisiwani, Tenge na Liwiti, Bonde la sungura, Tembo Mgwaza, Temeke, Mpogo, Minazi Mirefu, Kigilagila, Kiwalani upo katika hatua za awali za utekelezaji upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Kiasi cha Sh. 79,275,659,457.00 kinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa miradi hiyo.
Aidha; Ujenzi wa majengo 3 ya Ofisi za miradi katika Manispaa ya Temeke, Ilala na Kinondoni, umefanyika ili kuweza kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na Miundombinu kwa Jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake umegharimu kiasi cha shilingi 3,987,636,000/=.
Miradi ya ujenzi wa barabara iliyotekelezwa na Halmashauri
Miradi ya barabara iliyotekelezwa na Halmashauri kuanzia Januari 2016 kabla ya TARURA kuanza rasmi jukumu hilo ni kukamilisha ujenzi wa Barabara za kiwango cha lami km 10.6, changarawe km 132.1, mifereji ya mvua km 1.85 na udongo km 150, madaraja 4, karavati 14, matengenezo ya mara kwa mara km 64.6, taa 150 katika vituo vya basi vya simu 2000, Zanaki na Jamhuri pamoja na Vivuko vya waenda kwa miguu 2. Utekelezaji wa miradi hii iliyokamilika ni shilingi 15,342,028,000/=
.
Miradi iliyotekelezwa na DART
Katika kukabiliana na changamoto ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) tayari wamekamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza km 20.9 ambao utoaji huduma ulianza rasmi Juni, 2016. Aidha, Mradi huuulizinduliwa rasmi na Mhe. Dr John Pombe Joseph Magufuli. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 25 Januari, 2017.
Kuanza kwa utekelezaji wa Mradi kumesaidia kurahisisha huduma ya usafiri ambapo hadi sasa watu tarkriban 200,000 hupata huduma ya usafiri kwa kila siku na tayari zaidi ya watu 1000 wamepata ajira kupitia Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)
Usanifu wa awamu ya II na III umekamilika ambao umegharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 289.91. Ujenzi wa awamu ya II ambao utajumuisha Kituo Kikuu katika maeneo ya Mbagala na barabara za juu (flyover) unatarajia kuanza rasmi mwishoni mwa mwaka 2018 fedha za mradi huo zimepatikana (Dola za Kimarekani Milioni 141.71)
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Benki ya Dunia inaendelea na jitihada za kukamilisha usanifu wa awamu ya IV, V na VI wa mfumo wa DART ili kuweza kukamilisha ujenzi wa barabara zote kwa ujumla km 141.1.
Jedwali Na.23: Utekelezaji wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) katika Jiji la
Dar es Salaam Januari 2016 hadi Juni, 2018.
Awamu |
Jina |
Urefu (km) |
Maelezo |
I |
Barabara ya Morogoro (Kimara – Kivukoni), Barabara ya Kawawa (Morocco – Magomeni), Msimbazi – Kariakoo.
|
20.9 |
Utoaji huduma ulianza Mei, 2016 na huduma inaendelea kutolewa.
|
II |
Barabara ya Kilwa, Kawawa, Magomeni – Chang’ombe
|
20.3 |
Zabuni za ujenzi wa kumpata Mkandarasi zimetangazwa tarehe 12 Februari, 2018 (Majengo) na tarehe 05 Mei, 2018 (Barabara); Ujenzi unatarajia kuanza Mwaka huu 2018. Aidha Fidia inatarajiwa kulipwa kabla ya kuanza ujenzi.
|
III |
Barabara ya Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Azikiwe
|
23.6 |
Usanifu umekamilika
|
IV |
Barabara ya Bagaomoyo – Tegeta Sam Nujoma,
|
25.9 |
Usanifu unatarajia kuanza kufanyika kupitia Benki ya Dunia
|
V |
Barabara ya Mandela na Barabara mpya
|
22.8 |
Usanifu unatarajia kuanza kufanyika kupitia Benki ya Dunia
|
VI |
Barabara ya Mwai Kibaki na Barabara mpya mbili.
|
27.6 |
Usanifu unatarajia kuanza kufanyika kupitia Benki ya Dunia
|
|
JUMLA
|
141.1 |
|
Mafanikio ya Mradi wa DART
Katika kipindi cha Mwaka 2016/17- Mei 2018 mradi wa umepata mafanikio yafuatayo :-
Kuanza rasmi tarehe 10 Mei, 2016 kutolewa kwa Huduma ya Mpito kupitia mtoa huduma kampuni ya UDART wakazi wamenufaika na huduma Idadi ya abiria imeongezeka kutoka wastani wa 76,000 kwa Mwaka 2016 hadi 200,000 mwaka, 2018;
Huduma hii imepunguza msongamano wa magari barabarani katika eneo la Mradi awamu ya kwanza Kimara na Kivukoni ilikuwa ikichukua zaidi ya saa mbili kwa kutumia mabasi ya DART inachukua dakika 40 tu na hivyo kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku;
Mradi umefanikiwa hadi sasa umetoa ajira kwa watu zaidi ya 1,000 ikihusisha madereva, mafundi wa karakana, watumishi wa UDART, Watumishi wa kampuni ya ukusanyaji wa nauli; ulinzi na usafi wa vyoo, maegesho, madaraja ya watembeao kwa miguu katika mfumo wa DART;
Mradi umetoa fursa za kibiashara katika ushoroba wa mradi wa DART awamu ya kwanza ikiwemo fursa ya maegesho ya magari katika eneo la Kimara Mwisho;
Wafanyakazi na wafanyabiashara wanawahi kufika kazini na hivyo kuongeza tija na ufanisi. Kwa upande wa wanafunzi wameondokana na adha ya kunyanyaswa kwenye daladala;
Mabasi yanayotumika kwenye mfumo wa DART yana injini ambazo ni rafiki kwa mazingira;
Walemavu, akina mama wajawazito na wazee wamepewa kipaumbele katika mfumo wa DART;
Mradi umesadia kuboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam; na
Mradi umefanikiwa kupata tuzo mbili za Kimataifa kuhusu utunzaji Mazingira na Usafiri endelevu.
Ibara ya 39 (i) Vivuko (iv – v) Kuimarisha Usafiri wa Majini katika Mito, Maziwa na Bahari ili kufanya barabara kuwa na kiunganishi cha uhakika kwa kutekeleza miradi ifuatayo: -
Katika kuboresha usafiri Jijini Dar es Salaam na kupunguza msongamano, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wamenunua kivuko cha MV Kazi, kivuko hicho kinatoa huduma kati ya Wilaya ya Kigamboni na maeneo ya Kati (CBD) ya Jiji la Dar es Salaam.
Ibara 41 (a, b, c & i) Kushirikiana na sekta binafsi, kuendelea kuboresha huduma za uchukuzi katika Bandari ya Dar es Salam kwa kuanza kufanya yafuatayo;
Kuanza Ujenzi wa gati Na.13 na 14, kukamilisha uboreshaji wa gati Na 1-7 ili kuimarisha utoaji wa huduma, Kuanza ujenzi wa gati la kushusha magari (RoRo) katika Bandari na Kuboresha mfumo wa uondoshaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza kiwango cha utendaji kwa kuweka mfumo wa ‘electronic window System’ na kufunga mita za kupima mafuta.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania - Dar es Salaam; umefanya upanuzi wa Bandari kwa kuongeza kina kuanzia Gati namba 1– 7; kujenga Ro-Ro Berth ambayo kwa sasa ipo kwenye ujenzi kwa 40% pia inategemewa kukamilika Disemba, 2018. Sambamba na hayo Gati namba 1 inategemewa kukamilika Novemba, 2018.
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania – Dar es Salaam; imeweza kununua Forklift zenye uwezo wa kubeba kati ya tani 3 - 5 jumla ishirini na nane (28), na Forklift zenye uwezo wa kubeba tani 25 - 45 jumla nane (8); Mobile Crane moja (1) ya kubeba 90T, Patrol Boat moja (1), Tug Boat moja (1) yenye uwezo wa kuvuta meli zenye uzito mkubwa.
Ibara 41 (b) Kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya Jengo la Tatu la Abiria (Terminal III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kuanza ujenzi wa awamu ya pili ya Jengo la Tatu la JNIA;
Mamlaka ya viwanja vya ndege kwa kushirikiana na TANROADS wanaendelea na ujenzi wa jengo la abiria (Terminal III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambapo jengo linatarajia kutumika ifikapo Mei, 2019. Upanuzi wa Uwanja huo wa Ndege wa Kimataifa (terminal III) hususan njia za ndege zimekamilika kwa 60%, ujenzi wa Majengo ya Abiria unaendelea vizuri na kwa sasa upo 30% ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2019. Gharama ya upanuzi huo ni kiasi cha USD 4,506,222.22 na Tsh. 1,468,000,000/= Aidha, wameshakamilisha zoezi la kuhamisha Kaya 59. Aidha viwanja 537 vimehakikiwa kwa ajili ya kukamilisha awamu ya pili ya kuhamisha wananchi ili kupisha upanuzi wa kiwanja cha Ndege.
Mapokezi ya Ndege za ATCL
Serikali imenunua ndege sita ambapo hadi Juni, 2018 Ndege tatu zimekwishapokelewa kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam. Ndege zilizopokelewa ni aina ya Bombardier Dash 8 Q 400 zenye uwezo wa kupakia abiria 76. Uzinduzi na mapokezi ya Ndege hizo ulifanywa na Mhe John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndege ya kwanza ilipokelewa tarehe 20 Septemba, 2016 na ya tatu Tarehe 02 Aprili, 2018. Ndege zingine tatu zinategemewa kuwasili hivi karibuni ni ndege mbili za aina ya CS 300 zenye uwezo wa kupakia abiria 160 na moja kubwa aina ya Boeing 787 – 8 Dreamliner yenye uwezo wa kupakia abiria 240.
Ibara ya 41 a (i); Kwa kushirikiana na sekta binafsi kuanza ujenzi wa reli zifuatazo kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) awamu ya kwanza kuanzia Dar es Salaam
Kupitia Shirika la Reli (TRC) ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha “Standard Gauge” kwa awamu umeanza. Ujenzi kwa kipande cha kwanza DSM - Morogoro (Km 300) tayari umekwishaanza tangu Februari, 2017 na upo katika hatua mbalimbali. Ujenzi huo unategemewa kukamilika Novemba, 2019. Hadi mwezi Juni, 2018 kiwango kilichofikiwa ni asilimia 12.9 ya ujenzi wote, aidha katika ujenzi huo ulioanzia Jijini Dar es Salaam, nguzo 17 kati ya nguzo 100 zilizoko kwenye urefu wa mita 337 zimesimikwa kwa ajili ya daraja la Jijini Dar es Salaam litakalokuwa urefu wa takriban kilometa 3. Ujenzi wa nguzo hizo unategemewa kukamilika mwezi Mei, 2019.
Shirika la Reli Tanzania (TRC)
Ibara ya 41 (d) Kuendelea kuboresha usafiri wa Reli Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano.
Serikali kupitia Shirika la Reli imeanzisha huduma ya usafiri wa treni Jijini na kukarabati njia zilizokuwepo za kutoka Dar es Salaam - Ubungo na kuanzisha usafiri wa treni kati ya Stesheni ya Dar es Salaam na Pugu unaosafirisha takribani wasafiri 25,000 kwa siku. Huduma hii ya usafiri imesaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa wasafiri waendao Pugu kupitia maeneo ya Banana na Gongo la Mboto.
Sambamba na hilo Shirika la Reli limemwajiri Mshauri elekezi kampuni ya GIBB ya kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia mpya za reli kwenda maeneo ya Pugu kupitia uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Mbagala/Chamazi, Luguruni/Kibaha na Bunju/Kerege/Bagamoyo, ambapo kazi yake ipo katika hatua za mwisho. Ukarabati wa njia hii utasaidia kwa kiwango kikubwa kusafirisha abiria pamoja na mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Bara na nchi jirani kwa urahisi zaidi na kwa bei nafuu sambamba na kupunguza msongamano wa magari ya abiria Jijini Dar es Salaam.
Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA)
Serikali kupitia TAZARA ilifanya maboresho ya huduma kwa kuanzisha usafiri wa treni kati ya Stesheni ya Dar es Salaam na Mwakanga ili kukabiliana na changamoto ya msongamano barabarani katika Jiji. Kati Januari, 2016 hadi Juni, 2018 jumla ya abiria 5,853,710 walisafirishwa kati ya Stesheni za TAZARA na Pugu Mwakanga. Huduma hii ya usafiri imesaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani.
Aidha, ilifanya ukarabati wa Km 20 za reli ya TAZARA zilizopo Dar es Salaam, mabehewa ya abiria na mizigo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa