Seksheni hii ina lengo la kusaidia au kuwezesha utoaji huduma za uendelezaji wa Elimu ikijumuisha usimamizi wa elimu ya awali, msingi, sekondari, elimu ya watu wazima na inayotolewa katika njia isiyo rasmi; na mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Seksheni hii inaongozwa na Katibu Tawala Msaidizi ambaye pia ni Afisa Elimu wa Mkoa ambaye anawajibika kwa Katibu Tawala wa Mkoa.
Idadi ya watu katika Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa sababu ya shughuli za Viwanda na Biashara zinazofanyika. Mkoa una Taasisi nyingi kuliko Mikoa mingine. Kwa ajili hii uwiano wa watoto nao ni mkubwa kuliko Mikoa mingine. Hali hii inasababisha idadi kubwa ya wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkoa una jumla ya madarasa 494 ambayo yako kwenye shule mbalimbali za Serikali na hata hivyo, Sekta binafsi imeweza kuanzisha madarasa hayo pekee bila ya kuyaunganisha na Shule binafsi . Idadi hii ya madarasa bado hailingani na idadi ya shule za Msingi zilizopo. Hali hii inasababishwa na ukosefu wa maeneo ya kujenga madarasa hayo, kwa kuwa shule nyingi ziko Mjini na maeneo ya Shule ni madogo. Wanafunzi wa Elimu ya awali wanahitaji eneo la kutosha kwa kuwa hujifunza kwa vitendo zaidi ambavyo huhitaji nafasi kubwa. Uongozi wa Mkoa unaendelea kuzishauri Halmashauri kujenga majengo ya ghorofa ili kuongeza idadi ya madarasa ya Elimu ya awali na maeneo mengine yaachwe wazi kwa elimu ya vitendo.
Sekta binafsi ina jumla ya shule za awali 182 ambazo zinatoa Elimu ya awali kwa lugha ya Kingereza (English Medium). Katika Shule hizi elimu hutolewa kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
Kwa sasa Mkoa una jumla ya shule za Msingi 546 kati ya hizo 355 ni za Serikali na 191 zisizo za Serikali.
Wapo watoto ambao kwa sababu mbalimbali hawakupata bahati ya kupata elimu ya msingi katika umri unaostahili. Kwa kuelewa kuwa elimu ni haki ya msingi na ya muhimu kwa kila mototo, serikali ilianzisha mpango wa elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA). Mpango huu umegawanywa katika makundi mawili yaani kundi rika la kwanza kwa watoto walio kati ya miaka 10-13 na kundi rika la pili lenye vijana wa miaka 14-18. Vijana hao husoma kwa miaka 2-4 kisha wanafanya mtihani wa darasa la IV.Wanaofaulu hujiunga na elimu ya mfumo rasmi na baadhi yao ambao walidondoka njiani kisha kujiunga na MEMKWA huruhusiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wakifaulu huendelea na elimu ya sekondari.
Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya vyuo 11 vya ufundi stadi vinavyoendeshwa na Halmashauri ambapo wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi ambao hawakupata bahati ya kujiunga na masomo ya Sekondari wanapatiwa mafunzo ya miaka miwili katika fani mbalimbali kama vile Useremala, Uashi, Umeme na Ufundi Chuma nk. Vyuo vya Ufundi na Wanafunzi wanaojiunga wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulianza kutekelezwa Mkoani kuanzia mwaka 2001. Kutokana na mafanikio haya, Mkoa umeweza kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na pia kununua vitabu na vifaa mbali mbali vya kufundishia.
Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya 1994 ulikuwa na Shule za Sekondari 7 tu, ambazo ni Kisutu, Jangwani, Kibasila, Forodhani, Pugu, Azania na Zanaki. Idadi hii iliuweka Mkoa huu katika nafasi ya mwisho Kitaifa katika kuwa na idadi ndogo ya Shule za Sekondari ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaofaulu. Hali hiyo ilisababishwa na Mkoa kutokujenga Shule za Sekondari kama Mikoa mingine. Mkoa uliweka mikakati madhubuti ya kujenga shule za Sekondari. Hadi kufikia mwaka 2013 Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya shule za sekondari za Serikali 135 na 176 zisizo za serikali.
Ilani ya Uchaguzi inaelekeza kuwa suala la kufuta ujinga miongoni mwa watu wazima lipewe umuhimu na msukumo mpya. Mwaka 2014 jumla ya wanakisomo 9,415 wamesajiliwa katika madarasa ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
Changamoto kuu zinazokabili Elimu katika Mkoa huu ni upungufu mkubwa wa shule za sekondari za Serikali. Kuna jumla ya shule za msingi 546 ambazo hutegemea shule za sekondari za Serikali 133 . Hivyo kusababisha mrundikano mkubwa wa Wanafunzi katika shule za sekondari za Serikali. Upo pia upungufu wa vyumba vya madarasa 4,314 na madawati 76,029 kwa shule za msingi na vyumba vya madarasa 1,020 na madawati 35,420 kwa shule za sekondari za Serikali. Aidha kati ya shule za serikali 124 zilizojengwa kwa nguvu za wananchi, shule 77 ziko pembezoni na 47 ziko mjini. Wakati huo huo wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya msingi hutokea mjini. Hivyo kusababisha wanafunzi wengi wanaofaulu kutoka shule za msingi za mjini kukosa nafasi katika shule za sekondari zilizokaribu. Katika utekelezaji wa Mkakati wa Matokeo Makubwa sasa (BRN) tumetoa kipaumbele zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari yakiwemo madarasa, madawati na nyumba za walimu na mabweni kwenye shule za sekondari zilizoko pembezoni ili kuwawezesha walimu na wanafunzi wanaofundisha na wanaosoma katika shule hizo kuishi shuleni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa