HALI YA UTOAJI HUDUMA YA MAJISAFI, UONDOAJI MAJITAKA,
MIPANGO ILIYOPO NA MIRADI INAYOEENDELEA
MKOA WA DAR ES SALAAM HADI DESEMBA, 2018
HUDUMA YA MAJI
Mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam hadi mwezi Novemba, 2018 ni wastani wa lita milioni 544 kwa siku ambapo uwezo wa uzalishaji ni lita milioni 502 kwa siku. Vyanzo vikuu vya maji haya ni Mto Ruvu (88%), Mto Kizinga (03%) na visima virefu (09%). Maji yanayozalishwa kwa sasa yanakidhi mahitaji kwa asilimia 75 ya wakazi wa Jiji. Takriban asilimia 40 ya eneo la Mkoa halina mtandao wa mabomba ya DAWASA ambapo huduma hupatikana kupitia Visima vya Taasisi na watu binafsi, huduma hii huchangia asilimia 16 ya mahitaji.
Maeneo machache (20%) yaliyopo hasa katika Wilaya ya Kinondoni, Ilala na Ubungo hupata huduma ya maji kwa saa kati ya 20-24 wakati zaidi ya asilimia 40 hupata maji kwa mgawo wa wastani wa saa kati ya 8-16 kwa siku.
Eneo kubwa la Wilaya za Temeke na Kigamboni ndilo lenye kiwango cha chini ya asilimia 10 ya upatikanaji wa mtandao wa mabomba. Maeneo haya yanatarajiwa kupata huduma ya maji kutoka mradi mkubwa unaoendelea hivi sasa wa visima virefu 20 vya Kimbiji na Mpera.
Jitihada za kuongeza mtandao wa Majisafi zinaendelea ili watu wengi zaidi waweze kunufaika. Hadi kufikia mwezi Novemba, 2018 asilimia 75 ya wakazi waishio kwenye Mitaa katika Mkoa wa Dar es Salaam wanapata huduma ya majisafi na salama kupitia miradi ya maji iliyopo.
1.2 Hali ya Uondoshaji Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam
Mfumo (Central sewerage system) wa kuondosha Majitaka uliopo Jijini Dar es Salaam unahudumia asilimia 10 tu ya wakazi wote wa Jiji. Mifumo mingine ipo Lugalo, Chuo Kikuu cha DSM, Mwenge, Kijitonyama, Mikocheni, Kurasini, Buguruni, Uwanja wa Ndege, Airwing, Barabara ya Nyerere (Tazara), Vingunguti na Ubungo. Mifumo hii inamwaga majitaka katika mabwawa yaliyoko maeneo hayo.
Maeneo yasiyo na mfumo rasmi wanatumia vyoo vya shimo (Pit latrine) asilimia 70 na mashimo ya choo (septic tanks) asilimia 20.
Matarajio ya Mkoa ni kutoa huduma ya Majisafi na salama kwa asilimia 95 ya wakazi wa Jiji na asilimia 30 uondoshaji wa Majitaka katika Mkoa wa Dar es Salaam ifikapo 2020.
1.3.1 Mipango Kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) inayotekelezwa na Halmashauri za Manispaa.
Hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea kutekeleza jumla ya miradi 18 kati ya 41 ya visima vya maji iliyopangwa, katika Manispaa ya Ilala, Kigamboni, Kinondoni, Temeke na Ubungo chini ya mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji. Kati ya miradi hiyo, 13 imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi (Pugu Kajiungeni, Kipunguni B, Makongo Mbuyuni, Kivule, Goroka, Mianzini, Kizinga Bughidad, Mashine ya Maji, Kibwegere, Mpiji-Magohe, Mbuyuni, Mamboleo B na Mabatini). Aidha, miradi 5 ya maji ya Chambewa, Kibene, Malimbika, Kizuiani na Mbezi Makabe, utekelezaji wake unaendelea.
Katika kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu, miradi yote inaendeshwa na wananchi wenyewe kupitia Vyombo vya Watumiaji Maji/Vikundi vinavyoundwa kisheria. Hadi kufikia mwezi Desemba, 2018, Mkoa una jumla ya vyombo vya Watumia Maji (COWSOs) 81 vilivyosajiliwa kisheria na 53 mchakato wa kusajili unaendelea. Aidha, miradi ambayo inatumia mtandao wa DAWASA uendeshaji wake unakuwa chini ya DAWASA.
1.3.2 Miradi Mingine inayotekelezwa kwenye Halmashauri
Kupitia bajeti za Halmashauri, Own Source, na Wadau wengine (UNICEF, LGCGD, BTC, WATER AID, Africa Relief, African Muslim Agency-AMA, Food Aid Counterpart na mfuko wa Jimbo) Halmashauri zote tano zinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika maeneo yao kama ifuatavyo: -
Manispaa ya Ilala
Jumla ya Miradi 12 inatekelezwa katika maeneo ya Pugu Bangulo, Kinyerezi, Pugu Kichangani, Ulongoni A, Lada, Lubakaya, Lukooni, Segerea, Kitonga, Kipera, Mtambani na upanuzi wa mradi wa Pugu Kajiungeni kwenda Kinyamwezi, Mustafa na Viwege ujenzi wake umekamilika. Wananchi wapatao 45,000 wananufaika na huduma ya maji inayotolewa katika maeneo hayo.
Miradi 2 katika Mitaa ya Kisukuru na Mkera ujenzi wake unaendelea na umefika asilimia 95.
Manispaa ya Kigamboni
Mradi wa Mwasonga-Kisarawe II ujenzi wake umekamilika na umeanza kutoa huduma ya majaribio. Wananachi zaidi ya 7500 wananufaika na huduma ya maji inayotolewa.
Miradi 5 ya Minondo Somangila, Mkwajuni na Gezaulole ujenzi wake unaendelea. Wananchi wapatao 18,750 wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji itakayotolewa.
Uchimbaji wa visima 2 na ujenzi wa miundombinu katika Mitaa ya Sara na Lingato unaofanywa na Shirika la African Muslim Agency upo katika hatua za ukamilishaji.
Manispaa ya Kinondoni
Jumla ya Miradi 3 ya Makongo Juu, Kigogo Buyuni, Kigogo Kati na Shule ya Msingi Changanyikeni imekamilika. Wananchi wapatao 28,000 wananufaika na huduma ya maji inayotolewa.
Miradi 2 ya Mbezi Ndumbwi na Mbezi Mtoni ipo katika hatua za majaribio. Wananchi wapatao 2400 wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji itakayotolewa.
Manispaa ya Temeke
Jumla ya Miradi 3 ya Kurasini-Mvinjeni, Buza na Makuka ujenzi wake imekamilika. Wananachi zaidi ya 7000 wananufaika na huduma ya maji inayotolewa. Aidha, mradi wa maji Mkondogwa umekamilika na umeanza kutoa huduma kwa majaribio.
Mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika kata tatu maeneo ya Kibondemaji unaotekelezwa kwa msaada wa Shirika la Water Aid/PDF ujenzi wake umekamilika na unatoa huduma kwa Wananchi kwa wananchi wapatao 32,000.
Ujenzi wa mfumo wa kutibu Majitaka (DEWATs) katika eneo la Toangoma unaotekelezwa kwa msaada wa Shirika la Water Aid/PDF, ujenzi wake umekamilika, na unaendelea kutoa huduma kwa Wananchi. Jumla ya Wananchi wapatao 93,000 wanahudumiwa na Mradi huu.
Ujenzi wa mfumo wa kutibu Majitaka (DEWATs) katika eneo la Temeke Wailes unaotekelezwa kwa msaada wa Shirika la BORDA, ujenzi wake unaendelea, kwa sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji.
Manispaa ya Ubungo
Jumla ya Miradi 4 ya Makurumla mnara wa Voda, Makurumula Sisi kwa Sisi, Nzasa A na King'azi imekamilika na inatoa huduma kwa Wananchi wapatao 11,100. Aidha, upanuzi wa mradi wa King’azi A, ukihusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa wa lita 90,000 na litakalohudumia wakazi wapatao 15,400 upo katika hatua za majaribio ya tanki kuangalia kama halivuji.
Miradi 2 ya Matosa na Hondogo Gogoni ujenzi wake unaendelea, kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa tanki, nyumba ya Pampu na ulazaji wa mabomba.
Ujenzi wa mfumo wa kutibu Majitaka (DEWATs) katika eneo la Mburahati/Barafu, unaotekelezwa kwa msaada wa Shirika la BORDA, kwa sasa upo katika hatua ya majaribio.
Maelezo ya kina kuhusu mipango iliyopo na miradi mbalimbali inayoendelea yanapatikana kwenye Jedwali Na I.
1.3.3 Miradi Mikubwa Inayotekelezwa na DAWASA
Na. |
KAZI |
HATUA ILIYOFIKIWA |
1
|
Mradi wa visima virefu 20 Kimbiji na Mpera na Uchimbaji wa Visima vya Majaribio.
Lengo la mradi ni kuzalisha lita milioni 260 za maji kwa siku |
Hadi sasa visima 19 vimechimbwa na tekelezaji wake umefikia asilimia 87.5. Maandalizi kazi za kuendeleza mradi kwa awamu yanaendelea.
Visima vya maeneo ya Mpera vitahudumia wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Chanika, Luzando, Pugu, Mpera, Chamanzi, Kitunda, Ukonga, Kinyerezi, na Uwanja wa Ndege Visima vya maeneo ya Kimbiji vitahudumia wakazi wa maeneo ya Temeke, Kisarawe, Kibada, Kimbiji, Kigamboni, Tuangoma, Mkuranga, Kongowe, Mbagala, Kurasini, Mtoni, Tandika, Keko na Chang’ombe. |
2
|
Mradi wa Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza majisafi.
Lengo la mradi ni kuongeza mfumo wa usambazaji maji na kuunganisha wateja wote walioko katika maeneo yasiyo na mtandao na yale yatakayopata maji kutokana na upanuzi wa mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu. |
Hadi sasa kazi imefika asilimia 94.6. Kazi ya ulazaji mabomba na kuunganisha Wateja Maeneo ya Salasala na Wazo imekamilika. Maeneo ya ya Changanyikeni na Bunju hatua za ukamilishaji zinaendelea. Mfumo wa usambazaji maji katika maeneo ya Changanyikeni na Bunju unaendelea kutekelezwa kupitia mradi wa usambazaji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha maeneo ya Mpiji, Bunju, Mabwepande, Boko, Mbweni, Tegeta, Ununio, Wazo, Salasala, Kinzudi, Matosa, Mbezi Juu, Goba, Changanyikeni, Makongo, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Msakuzi, Makabe, Malamba mawili na Msigani. |
3
|
Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na mtandao DAWASA (Off grid water supply and sanitation)
Lengo ni kuwapatia Wananchi wapatao 100,000 huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, katika maeneo ambayo hayana mtandao wa Majisafi na Majitaka. Mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. |
Mradi utahusisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na mtandao rasmi wa mabomba, mifumo midogo (50) ya kukusanya na kuchakata Majitaka (DEWATs) na ujenzi wa vyoo. Utekelezaji wa Programu hii ni kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia Julai 2017.
Kazi ya Utambuzi wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya majisafi, majitaka na vyoo inaendelea. |
4
|
Mradi wa Uboreshaji Mfumo wa Uondoaji Majitaka (Upanuzi wa Miundombinu ya majitaka na ujenzi wa mfumo mpya)
Lengo la mradi huu ni kuongeza upatikanaji wa huduma ya Majitaka kwa wakazi wa Jiji la DSM kutoka asilimia 10 ya sasa hadi kufikia asilimia 30 ifikapo Desemba 2020. |
Mradi huu utahusu ujenzi wa mitambo mitatu ya kisasa ya kusafisha majitaka itakayojengwa katika maeneo ya Jangwani (200,000 m3/siku), Kurasini (11,000 m3/ siku), na Mbezi Beach (16,000 m3/siku).
Kazi zitakazofanyika chini ya Mradi huu ni pamoja na upanuzi wa mfumo wa majitaka katika maeneo ya Katikati yaJiji, ujenzi wa mfumo mpya Ilala, Magomeni hadi Ubungo,Sinza, Kinondoni, Mwananyamala, Oysterbay, Masaki, Msasani, Kawe, Mbezi Beach, Kurasini, Keko, Chang’ombe na Temeke. |
5
|
Miradi ya Visima vya dharura katika maeneo yasiyo na maji ya bomba
Lengo la miradi hii ni kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza adha ya maji katika maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA |
Uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu katika maeneo yasiyo na maji ya bomba unaendelea. Miradi hii ni hatua ya dharura ili kupunguza kero ya maji wakati miradi mikubwa ya kuongeza maji inaendelea kutekelezwa. Jumla ya Miradi 13 ya visima inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji.
|
2.0 Mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma ya maji baada ya kukamilika kwa Miradi mbalimbali (2015-2018).
Kukamilika kwa Mradi Mkubwa wa Ruvu Chini ambao umeongeza upatikanaji wa Maji kutoka Lita Milioni 182 na kufikia lita milioni 270. Mradi umekamilika Mwezi Machi, 2016 na unatoa huduma ya maji kwa Wananchi. Mradi huu umepunguza kero ya maji kwa wakazi wanaotumia maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini unaohusisha maeneo ya Bagamoyo na vitongoji vyake, Bunju, Mabwepande, Boko, Tegeta, Kunduchi, Mbezi Beach, Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo, Chuo Kikuu, Mikocheni, Msasani, Masaki, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo, Kigogo, Buguruni, Ilala, Maeneo ya Katikati ya Jiji la DSM pamoja na Kurasini na Bandarini.
Kukamilika kwa Mradi Mkubwa wa Ruvu Juu ambao umeongeza upatikanaji wa Maji kutoka Lita Milioni 82 na kufikia lita milioni 196. Mradi umekamilika Mwezi Aprili, 2017 na unatoa huduma ya maji kwa Wananchi. Kukamilika kwa mradi huu kumepunguza kero na uhaba wa maji katika miji ya Mlandizi na Kibaha pamoja na maeneo ya Kiluvya, Kibamba, Changanyikeni, Mbezi, Kimara, Kibangu, Makuburi, Tabata, Segerea, Vingunguti, Airport, Ukonga, Kipawa na Katikati ya Jiji la DSM.
Kukamilika uchimbaji wa visima 19 kati ya visima 20 vya Kimbiji na Mpera ambavyo vitaongeza upatikanaji wa maji kwa lita milioni 260;
Kukamilika kwa miradi ya Visima 15 vya ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji (BTC) ambayo inahudumia zaidi watu 250,000;
Kukamilika kwa miradi ya vijiji 10 kupitia mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo inahudumia zaidi watu 120,000;
Kukamilika kwa miradi ya visima vya dharura vya DAWASA, Mapato ya ndani ya Manispaa, Mfuko wa Jimbo, Water Aid, TASAF, African Relief of Kuwait na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo inahudumia zaidi ya watu 230,000.
Matarajio ya Mkoa ni kuwapatia watu huduma ya Majisafi kwa asilimia 95 ya wakazi wote na uondoshaji wa Majitaka kwa asilimia 30 ifikapo mwezi Desemba 2020.
Changamoto kubwa katika utoaji wahuduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni kasi ndogo ya uwekezaji ukilinganishwa na kasi kubwa ya ongezeko la watu. Ongezeko kubwa la watu Jijini hasa kuanzia miaka ya 1980 kwa kiasi kikubwa limechangia katika kuongeza mahitaji ya maji. Changamoto zingine ni pamoja na: -
S/No
|
CHANGAMOTO
|
MIKAKATI
|
1
|
Upanuzi wa mtandao wa DAWASA kutokukidhi ya mahitaji wa wakazi wa Jiji
|
Mtandao wa kusambaza maji kutoka visima 20 vya Kimbiji na Mpera ukijengwa na Usambazaji inayoendelea ikikamilika itaongeza upatikanaji huduma kwa kiwango kikubwa
|
2
|
Upatikanaji wa maeneo ya
kujenga miundombinu |
Kuendelea kuwasiliana na Wadau ili kupata maeneo ya kujenga miundombinu ya maji na pia kutumia way leave zilizopo kwa kukubaliana na Taasisi husika
|
3
|
Ukuaji na ujenzi holela wa
makazi, |
Ushirikishwaji wa Jiji, Manispaa na Wizara ya Ardhi katika Upangaji wa Miji, Master Plan iwepo na izingatiwe wakati wa ujenzi wa Miradi
|
4
|
Wizi wa maji, uharibifu na wizi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka,
unachangia kiwango kikubwa cha maji yasiyolipiwa |
Kushirikiana na wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda miundombinu na kuzuia wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu na uchafuzi wa maji
|
5
|
Watumiaji maji kutokulipa
Ankara za maji kwa wakati, |
Kuweka dira za kulipia kabla ya matumizi (pre paid meters) kwa wateja wote, usomaji wa dira za maji kufanywa kwa kutumia vifaaa maalum vya kuchukua kumbukumbu (data loggers) ili kupata takwimu sahihi
|
6
|
Mfumo wa kuondoa majitaka haujafika maeneo mengi ya Jiji (unakidhi asilimia 10 tu)
|
Ujenzi wa miundombinu ya Majitaka kukidhi asilimia 30 ya mahitaji unahitajika
Mradi wa kujenga mifumo mikubwa 3 (Jangwani, Mbezi Beach na Kurasini) na Ujenzi wa mifumo midogo 50 ya kusafisha Majitaka chini ya Programu ya Maerndeleo ya Sekta ya Maji. |
7
|
Migogoro ya uendeshaji Miradi ya Maji ya Jamii inayosimamiwa na Jumuia za Watumia Maji (COWSOs).
|
Tathmini imefanyika kuona namna bora ya usimamizi wa miradi ya Jamii. Miradi inayotumia mtandao wa DAWASA na isiyo na utendaji mzuri, uendeshaji wake kuhamishiwa DAWASA. Hadi sasa miradi 20 ya Jamii shughuli zake za uendeshaji zimekabidhiwa DAWASA
|
8
|
Uchimbaji holela wa visima usiozingatia taratibu
|
Zoezi la kutambua na kusajili visima na kutoa vibali halali kwa wamiliki wa visima linaendelea. Zoezi linasimamiwa kwa kushirikiana na Ofisi za Bonde la Wami Ruvu.
|
4.0. Mwisho
Tunatoa wito kwa Wadau na watumiaji wa huduma ya maji Mkoa wa DSM kulipia Ankara za maji kwa wakati, kuepuka wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu ya maji, kulinda miundombinu iliyopo nainayojengwa ili huduma ya maji iwe endelevu. Aidha, ulinzi shirikishi wa vyanzo vya maji ni budi upewe kipaumbele katika ngazi zote, pia wananchi kutoa taarifaya ya uvujaji wa maji ili kuweza kupunguza upotevu wa maji.
"MAJI NI UHAI NA USAFI WA MAZINGIRA NI UTU"
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa