Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba amefanya ziara ya kutembelea miundombinu mbalimbali jijini Dar es salaam ikiwemo iliyoathiriwa na vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 29 na kuelekeza usafuri wa mwendokasi kurejea ndani ya siku kumi huku pia akiagiza kanisa la ufufuo na uzima kufunguliwa ili kutoa haki kwa waumini kuendelea na ibada
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika Mbezi mwisho wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam Dkt Mwigulu pamoja na kutoa pole kwa wananchi amesema usafiri huo wa mwendokasi ambao miundombinu yake imeharibiwa ni muhimu kwa wananchi hivyo ni lazima kufanyike maboresho ya haraka na urejee mara moja huku akielekeza wizara ya TAMISEMI kuwaamini wakandarasi wazawa kwenye ujenzi wa miradi ya barabara na maeneo mengine ili vijana wa kitanzania wapate ajira.
Aidha ameagiza watumishi wote wazembe na wala rushwa wasihamishwe vituo vya kazi bali wafukuzwe kazi kwani wapo vijana wengi wanaohitaji kupata ajira ambapo amewataka vijana kulinda nchi yao badala ya kushiriki katika vitendo vya uharibifu wa nchi yao huku akiwataka kuiamini tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia.
Akizungumzia suala la kanisa la ufufuo na uzima kufunguliwa Dkt Mwigulu amesema ni muhimu lifunguliwe na lipewe muda wa miezi sita ya matazamio kwani akifanya kosa kiongozi wa kanisa au msikiti si vyema kuwaadhibu waumini ambapo pia amezungumzia maelekezo ya Rais Dkt Samia kuwa sherehe za maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika 9 Disemba mwaka huu hazitakuwepo na fedha za maadhimisho hayo zitumike kuboresha miundombinu iliyoharibiwa siku ya uchaguzi mkuu.
Awali kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Waziri wa TAMISEMI Riziki Shemdoe amesema kuwa katika barabara ya kutokea katikati ya Jiji kuja kimara zaidi ya vituo 20 vya mwendokasi vimeharibika pamoja na mifumo muhimu ya ukataji tiketi jambo ambalo limesababisha usafiri huo kusitishwa kwa muda
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amezungumzia baadhi ya athari zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 29 na kuahidi kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa amani na kulinda nchi yao pia amesisitiza kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki bila kutoa rushwa ikiwemo vijana kupata mikopo na huduma zingime zikiwemo maji na afya kwani mambo hayo huchangia hasira na chuki za wananchi kwa serikali yao
Naye Waziri wa Mawasiliano na Tekinolojia ya habari ambaye pia ni Mbumge wa jimbo la Kibamba Anjela Kairuki na Waziri wa Uwekezaji Profesa Kilila Mkumbo pamoja na kuwashukiru wananchi na kutoa pole kutokana na vurugu zilozojitokeza siku ya uchaguzi wamewataka vijana kuwa wazalendo kwa Taifa na kuepuka kutumika na watu wasiokua na nia njema kwa Taifa huku wakipongeza kazi ya kuboresha huduma za jamii inayofanywa na serikali huku pia wakiomba stendi ya Magufuli itumike ipasavyo

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa