Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ametoa taarifa rasmi ya kuanza kurejea kwa huduma mbalimbali muhimu za kijamii katika Mkoa huo ikiwemo uingizwaji wa malori ya vyakula, usafiri wa mabasi ya mikoani pamoja na biashara ya nishati ya mafuta ya petroli na diseli kwenye vituo mbalimbali huku akipiga marufuku uuzwaji wa nishati hiyo ya mafuta kwenye vidumu
Kauli hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ni kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan la kuitaka mikoa yote nchini kuhakikisha huduma na shughuli za kijamii zilizosimama kutokana na tishio la kiusalama zinarejea mara moja.
Akizungumza Jijini Dar es salaam na waandishi wa habari RC Chalamila amesema wakati vyombo vya dola vikiendelea kuimarisha amani baada ya matukio ya vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyofanywa na baadhi ya vijana wakati wa uchaguzi, ameelekeza huduma zote kurejea ikiwemo ya vivuko kuelekea kigamboni,malori yanayosafirisha bidhaa, nishati ya mafuta, mabasi ya kwenda mikoani yaanze kazi kwa utaratibu maalumu.
Pia ameelekeza huduma za daladala,bajaji pamoja,na bodaboda kuendelea huku akikemea upandishaji wa bei za bidhaa kiholela na kwamba serikali haitosita kuchukua hatua
Aidha RC Chalamila amezungumzia usafiri wa Mwendokasi ambao miundombinu yake imeathiriwa na matukio ya uhalifu wakati wa uchahuzi ambapo amesema usafiri huo kwa njia ya kuelekea kimara na mbagala umesitishwa kwa muda wakati serikali ikifanya tathmini ya uharibifu huo pamoja na marekebisho ya miundombinu.
RC Chalamila ameitaka mamlaka ya usimamizi wa usafiri nchi kavu LATRA kutoa vibali vya muda kwa daladala za kwenda kutoa huduma za usafiri hasa kwa abiria wanaotokea mbezi na kimara kuelekea katikati ya jiji na ameweka msisitizo kwa daladala, bajaji na bodaboda kutotumia njia za mwendo kasi huku akiagiza kuwepo kwa kikao cha EWURA na wadau wa mafuta

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa