Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo July 12 amekabidhiwa Ofisi mbili za walimu Kati ya tano zinazojengwa na Ubalozi wa China nchini Tanzania kama sehemu ya kuunga mkono jitiada za Mkuu wa Mkoa katika kupatia ufumbuzi kero za Walimu.
RC Makonda amesema ofisi hizo za kisasa zina Chumba cha Mwalimu Mkuu, chumba cha Mwalimu Mkuu msaidizi, ofisi ya Mwalimu wa Taaluma, ofisi ya walimu wote, ukumbi wa mkutano, chumba cha mhasibu, karani, mapokezi,stoo,chumba cha kubadilishia nguo, chumba cha kuhifadhi vifaa vya michezo, mitihani pamoja na Vyoo na Bafu huku jengo likiwa na madirisha ya vioo, AC, TV Flat screen, Meza za kisasa, Makabati, Droo na viti vya kisasa.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya jengo iliyofanyika shule ya sekondari Makumbusho RC Makonda amesema kukamilika kwa ofsisi hizo kutatoa fursa ya upatikanaji wa madarasa matano yaliyokuwa yakitumiwa na walimu Kama ofisi ambapo kwa sasa yatarejeshwa kwa wanafunzi.
Aidha RC Makonda amesema kampeni ya ujenzi wa ofisi 402 za walimu ipo katika hatua nzuri na hivi karibuni atakabidhi ofisi 50 zilizokamilika kwaajili ya kuanza kutumika na walimu.
Hata hiyo RC Makonda amemshukuru Balozi wa China Bi. Wang Ke kwa kujenga ofisi hizo ndani ya muda mfupi na kusema hali hiyo itasaidia walimu kuwa na morali ya kazi na kusaidia ufaulu kuongezeka.
Pamoja na hayo RC Makonda amewaeleza walimu kuwa licha ya kuwatafutia mikopo ya viwanja vya bei nafuu, kupanda kwenye daladala na Treni bure bado anayo mipango mingi ya kuendelea kuwaboreshea mazingira ya kazi.
Kwa upande wake Balozi wa China Bi. Wang Ke amesema kuwa baada ya leo kukabidhi ofisi mbili za Shule ya Makumbusho na Kasulu iliyopo Ilala kwa sasa kinachofuata ni ujenzi wa ofisi tatu nyingine alizoahidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa