-Amshukuru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila leo Januari 22, 2025 ameongoza kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Hotel ya Four Points Posta Ilala.
RC Chalamila wakati anafungua kikao hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini hususani Mkoa wa Dar es Salaam " Mhe Rais ameunda timu ya watalaam wabobevu kupitia masuala ya kikodi kwa lengo la kuja na suluhu ya malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kodi kandamizi hii ni ishara ya dhamira njema ya Mhe Rais" Alisema RC Chalamila
RC Chalamila kupitia kikao hicho alitoa nafasi kwa wafanyabiashara kueleza changamoto na vikwazo vya kibiashara, ushauri, maoni pamoja na mapendekezo yao vilevile ufafanuzi wa maeneo ambayo yalikuwa yakilalamikiwa siku za nyuma kama yamefanyiwa kazi au la!
Aidha RC Chalamila amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Mkoa utaendelea kuweka mipango ya maendeleo ya kibiashara kupitia maoni na ushauri unaotolewa katika vikao vya mabaraza ya Biashara Mkoa pia amewataka kutumia vizuri fursa zilizoko ikiwemo kufanya biashara saa 24 pamoja na fursa za Uchumi wa bluu.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa Dkt Toba Nguvila amesema kikao hicho ni muhimu kwa masilahi mapana ya maendeleo ya Biashara katika kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa hivyo ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa pia kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kama inavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria katika ngazi ya Mkoa na wilaya zote tano.
Naye mwenyekiti wa Baraza la wafanyabiashara Mkoa Bwana Denis Chacha ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zao ambapo amesema watafanya kikao chao ili kutoa fursa zaidi za kueleza changamoto zao
Mwisho kikao hicho kimehudhuriwa na wafanyabiashara, wawekezaji, watalaam wa kutoka Wizara ya biashara, Sekretariati ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na makatibu Tawala wa Wilaya zote za Mkoa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa