-Apongeza Jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Kinondoni katika ukusanyaji wa mapato
-Asisitiza ubunifu na matumizi ya Teknolojia katika shughuli za ndani ya ofisi, ukusanyaji wa mapato na katika kuwahudumia wananchi
-Atoa Rai kujitokeza kwa wingi kupiga kura uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025
-Ataka kutolewa elimu zaidi kwa umma namna bora ya kuishi mjini (usafi)
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndg Abdul Rajab Mhinte amewataka wataalamu katika Mkoa huo kutumia zaidi maarifa kuliko nguvu katika ukusanyaji wa mapato.
Ameyasema hayo leo Septemba 10, 2025 kwa nyakati tofauti akiwa anaongea na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Katibu Tawala Mhinte amepongeza kwa ujumla jitihada zinazofanywa na Halmashauri hizo katika ukusanyaji wa mapato ambapo amezitaka kuongeza jitihada zaidi kwa kuwa Dar es Salaam ni jiji kubwa na lina vyanzo vingi vya mapato.
Aidha amesisitiza matumizi ya maarifa zaidi kuliko nguvu, hivyo amewataka kuwa wabunifu, matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku ndani ya ofisi na katika kuwahudumia wananchi hivyo "Ningefurahi zaidi kero nyingi za wananchi zitatuliwe katika ngazi za chini, pia wananchi wahudumiwe vizuri, lugha yenye staha itumike" Alisema Ndg Mhinte.
Sambamba na hilo Katibu Tawala amezitaka Halmashauri hizo kuwa na programu mbalimbali za elimu kwa umma hususani masuala yahusuyo usafi katika Jiji ambapo amesema wananchi waelimishwe namna nzuri ya kuishi mjini pia ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Octoba 29, 2025 katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Ndg Elhuruma Mabelya na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Bi Hanifa Hamza kwa niaba ya watumishi wemeahidi kuyafanyia kazi maagizo yote ya Katiba Tawala wa Mkoa pamoja na kuwa wabunifu zaidi katika nyanja mbalimbali kwa masilahi mapana ya wananchi wa Halmashauri hizo na Taifa kwa ujumla.
Ifahamike kuwa Katibu Tawala wa Mkoa Ndg Abdul Rajab Mhinte yuko katika ziara ya kujitambulisha katika Halmashauri zote za Mkoa huo toka apate uteuzi wa kuhudumu katika Mkoa huo ambapo Septemba 11,2025 anatarajia kukutana na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Kigamboni
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa