Maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani kwa Mkoa wa Dar es Salaam yameadhimishwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo katika Hospitali ya Sinza Palestina Jijini Dar es salaam.
Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori
Sherehe za maadhimisho hayo huendana na kumbukizi ya Muasisi wa uuguzi Duniani Frorence Nightingale ambaye ndiye kielelezo cha utumishi wa Uuguzi.
Chama cha wauguzi Tanzania tawi la Dar es Salaam kimeungana na waunguzi wengine ndani na nje ya Tanzania kuadhimisha siku ya leo tarehe 12/05/2018 katika hospitali ya Sinza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Sherehe hizo zimepambwa na Maandamano ya wauguzi wa Halmashauri za Manispaa tano yaani Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni na mwenyeji Ubungo.
Pia kulikuweko na maonesho ya utoaji wa huduma mbalimbali za kiafya kama vile upimaji wa UKIMWI, Uzito, na Magonjwa meningine mfano kisukari.
Wauguzi walipata fursa ya kumueleza mgeni rasmi mafanikio na changamoto wanazokutana nazo kila siku wanapotekeleza majukumu yao ya kiuguzi.
Zipo changamoto zilielezwa mfano Uhaba wa watumishi katika fani ya uuguzi, kutokupatikana kwa stahiki zao kama posho za masaa ya ziada lakini pia usalama mahali pa kazi na kazalika.
Mgeni rasmi alisikiliza mafanikio na changamoto za wauguzi na kutoa pongezi kwa kuwa wanachapa kazi vizuri na kuwahaidi Serikali ya awamu ya tano inawathamini wauguzi wake na ndio maana tayari imeshatoa kibali cha kuajiri watumishi katika sekta ya afya bila kusahau kwa kadiri uchumi utakavyoimarika ataongeza mishahara minono.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam mgeni rasmi amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote na Wakurugenzi kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili Wauuguzi.
Aidha Mgeni Rasmi Mhe Kisare Makori kwa kuthamini umuhimu wa maisha bora kwa wauguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam ameongoza harambee na kufanikisha kukusanya ahadi ya kiasi cha Tsh 4,050,000 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa Saccos ya Wauguzi huku ofisi yake ya Wilaya ikihaidi kutoa Tsh 1,000,000
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo hakuwa nyuma akahaidi kuchangia Tsh 1,000,000 kwa ajili ya Kutunisha mfuko wa Saccos hiyo yenye lengo la kuboresha maisha ya wauguzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa