Saturday 21st, December 2024
@Dar es Salaam
TAARIFA YA KAIMU MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KWA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZINGIRA DUNIANI, KUANZIA TAREHE 31 MAY HADI 5 JUNE 2018.
Ndugu wananchi
Tarehe 5 Juni, 2018 watanzania wote tutaungana na nchi mbalimbali duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yanaadhimishwa kutokana na uumuzi wa mwaka 1972 uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani kuwa kila tarehe 5 Juni ya kila mwaka itakuwa ni siku ya Mazingira. .
Ndugu wananchi
Kimataifa maadhimisho haya yana kaulimbiu isemayo “Beat Plastic Pollution”. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kuepuka uchafuzi wa Mazingira utokanao na plastiki. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya nchini India ni kutokana na nchi ya India kuweka juhudi katika kupunguza uchafuzi wa Mazingira utokanao na plastiki kwa kutumia mbadala wa plastiki na kurejeleza taka za plastiki. Aidha, India ni moja ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kurejeleza taka za plastiki ukilinganisha na nchi nyingi duniani.
Ndugu wananchi
Kitaifa maadhimisho haya yatafanyika Jijini Dar es Salaam, Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Mkaa Gharama; Tumia Nishati Mbadala”. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kupunguza matumizi makubwa ya Nishati ya mkaa ambayo yamesababisha kiasi kikubwa cha mistu yetu kuteketezwa. Takwimu zinaonesha kuwa mpaka mwaka 2017 kiasi cha hekta 46,942 za msitu kimekuwa kikiteketezwa kila mwaka kwa na matumizi makubwa yakiwa ni nishati ya mkaa. Inakadiriwa kuwa Jiji Dar es Salaam, linatumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka kiasi ambacho kinakadiriwa kuongezeka sana kutokana na ongezeko kubwa la watu kwa kila mwaka.
Ndugu Wananchi
Mkoa wa Dar es Salaam umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho haya kutokana na kuwepo kwa changamoto za uharibifu wa Mazingira unaotukumba, kama vile;- mafuriko; uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki; kubomoka kwa kuta za fukwe za bahari ya Hindi na kingo za mito yetu ya asili ongezeko la shughuli za kibinadamu; ongezeko la taka ngumu na matumizi makubwa ya nishati ya mkaa.
Ndugu wananchi
Matumizi makubwa ya nishati ya mkaa yamesababisha uharibifu mkubwa wa misitu ambao umechangia kuwepo kwa changamoto nyingine za Mazingira kwa Mkoa wetu. Mkoa wetu umekuwa ukikabiliana na mafuriko, mlipuko wa magonjwa ya binadamu na mazao, upotevu wa rutuba, upotevu wa mimea asilia, upotevu wa viumbe asilia, upungufu wa maji safi na salaama na uharibifu mkubwa kwa miundo mbinu ya kisasa na asilia. Hivyo, wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani itakuwa na, maonesho ya nishati mbadala ya mkaa na teknolojia zake. katika viwanja vya Mnazi mmoja kuanzia tarehe 31 Mei, hadi tarehe 5 Juni, 2018. Maonesho haya yatatoa fursa kwa jamii kuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kutumia nishati mbadala badala ya kuwa na matumizi makubwa ya Nishati ya Mkaa. Tarehe 3 Juni katika viwanja vya Zakhem Mbagala tutakuwa na utoaji wa zawadi kwa wadau wa mkoa huu watakaokuwa na teknolojia rahisi na endelevu ya kuzalisha nishati mbadala pamoja na wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa mazingira kwa mkoa wa Dar es Salaam. Sambamba na hilo wananchi wa mkoa huu watapata nafasi ya kuongea na vyombo vya habari moja kwa moja kuhusu masuala mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira. Tarehe 5 Juni, 2018 itakuwa ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mgeni rasmi atatoa zawadi kitaifa kwa wadau watakaokuwa na teknolojia rahisi na endelevu ya kuzalisha nishati mbadala pamoja na wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla, ninatoa wito kwa kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa ujumla kutumia fursa ya maadhimisho haya kujifunza matumizi bora ya nishati mbadala ili kuweza kuondoa mkoa wetu kwenye matumizi makubwa ya mkaa na kwa kufanya hivyo tutakua tumeoka misitu yetu.
Ndugu Wananchi
Kutokana na changamoto mbalimbali za mazingira zinazoikabili nchi yetu ukiwemo na mkoa wetu kwa ujumla maadhimisho haya yataambatana na Kongamao la Mazingira kuhusu suala la Mabadiliko ya Tabianchi na athari zake kiuchumi ambalo litafanyika tarehe 1 Juni, 2018 katika hoteli ya Hiyat Regency. Kongamano hilo litawahusisha wataalamu wa masuala ya Mazingira, Uchumi na Maendeleo pamoja na viongozi wa Serikali ambapo litajadili namna uchumi wa Tanzania unavyoathiriwa na Mazingira pamoja na mabadiliko ya Tabianchi.
Sambamba na hilo tutakuwa na Kongamano la viongozi wa madhehebu ya Dini mbalimbali litakalofanyika tarehe 2 Juni, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Kisenga Jengo la Hifadhi ya Mfuko wa Jamii (LAPF) Kijitonyama. Viongozi hao watajadili nafasi ya Imani na mazingira. Naamini baada ya kongamano hilo wananchi wa Mkoa huu wenye imani ya dini mbalimbali watahamasika kufanya juhudi katika kuhifadhi Mazingira ya maeneo yao.
Ndugu Wananchi
Mkoa huu umekuwa ukiathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi, ambapo athari zake ni kuongezeka ujazo wa bahari na mawimbi makubwa yanayosababisha kubomoka kingo za bahari. Wananchi wengi wa mkoa huu walio kwenye kingo za ufukwe za bahari ya Hindi wamepoteza mali zao. Ilikukabiliana na athari hiyo Serikali imefanya juhudi za kujenga ukuta huo kando ya barabara ya Barack Obama na eneo la chuo cha kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Kwa hali hiyo nawatangazia kuwa tarehe 5 Juni, 2018 siku ya Kilele cha maadhimisho haya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafanya ufunguzi wa ukuta huo. Wananchi mnaombwa kuhudhulia kwa wingi eneo la barabara ya Baraka Obama ili kushuhudia uzinduzi wa ujenzi wa ukuta huo.
Ndugu wananchi
Natumia nafasi hii kuwakaribisha mikoa jirani kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Aidha, nawaomba wananchi wa mikoa jirani kushiriki kwenye shughuli zote za maadhimisho zinazofanyika wakati wa wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira, hususani kwenda kwenye viwanja vya mnazi mmoja kuona na kupata elimu juu ya matumizi ya nishati ya mkaa mbadala na teknolojia zake. Nitoe wito kwa Wajasiliamali wote kwenda kwenye viwanja vya Mnazi mmoja kujifunza namna ya kuingia kwenye ujasiliamali wa kutengeneza Nishati ya Mkaa Mbadala tangu tarehe 31 Mei, hadi tarehe 5 Juni, 2018.
Mwisho, navipongeza vyombo vya habari ambavyo moja kwa moja vimeshaanza kazi nzuri ya uhamasishaji na ukuzaji weledi kwa wananchi juu ya kaulimbiu ya kimataifa na kitaifa ya siku ya Mazingira duniani. Na waomba muendeleze juhudi zenu za kuelimisha umma ili kujenga mahusiano endelevu na Mazingira. Natambua kuwa vyombo vya habari ni muhimili mhimu na mnayo nafasi na uwezo mkubwa wa kuifikia jamii katika kujenga Mazingira bora na Himilivu katika mkoa wetu. Nimalizie kwa kusisitiza kwamba, pamoja tunaweza
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Dar es Salaam
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Felix Lyaniva
KAIMU MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM
28/05/2018
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa