TAARIFA YA VITAMBULISHO VYA WAFANYABIASHARA WADOGO NA WATOA HUDUMA WADOGO.
Vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo ni vitambulisho vinavyotolewa kwa walengwa kupitia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli. Vitambulisho hivi vinatolewa vikiwa na lengo la kuwapatia utambulisho wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo katika biashara wanazozifanya na kuweza kutatua changamoto zao. Hii ikiwa ni pamoja na fursa ya kufanya biashara bila kubughudhiwa, kutambulika na watoa huduma wengine kama Taasisi za kifedha.
Walengwa haswa wa vitambulisho hivi ni wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara zenye patoghafi chini ya shilingi milioni nne.
Programu hii ya ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ilianza kutekelezwa mwaka jana 2019 ambapo lengo lilikuwa kuwafikia walengwa 376,000 ambao ni wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo Mkoani Dar es Salaam. Zoezi limefanikiwa ambapo mpaka sasa hivi walengwa 211,306 wameweza kufikiwa na kugawiwa vitambulisho hivyo ndani ya kipindi hiki. Zoezi hili bado linaendelea kufanyika katika Ofisi za Manispaa zote za Mkoa pamoja nao Ofisi za Watendaji wa Kata.
Fursa mbalimbali zimeweza kupatikana kwa wafanyabiashara wadogo kupitia zoezi hili la ugawaji wa vitambulisho ambapo mpango huu umewawezesha wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo kutambulika na kupata mikopo kwa kutumia vitambulisho vyao.
Kupitia ugawaji wa vitambulisho hivi vya wafanyabiashara wadogo kwa mwaka huu wa 2020, Mkoa unatarajia kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo kwa kuwapa elimu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali ili kuweza kukua kifikra, mitaji, kipato na hatimae kuweza kukidhi vigezo vya kulipa kodi na kuchangia pato la Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Vilevile upo mkakati wa kuzifikia Taasisi nyingi zaidi za kifedha ili kukipa thamani zaidi kitambulisho hiki na kiweze kutumika kama dhamana ya kupata mitaji kwa njia ya mikopo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa