
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amewataka wahariri na waandishi wa habari kufanya kazi yao bila upotoshaji wa taarifa hususani kwenye masuala yanayoweza kuleta taharuki kwenye jamii na kusisitiza kuwa Serikali Mkoani humo haikubaliani na matukio ya ya uhalifu ikiwemo utekaji.
Akizungumza katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es salaam leo Disemba 5, 2025 RC Chalamila amesema upotoshaji wa taarifa unaweza kuligharimu Taifa hasa nyakati zenye taharuki huku akitolea mfano wa matukio ya uchaguzi mkuu wa oktoba 29 ambapo ameeleza wazi kuwa Serikali imejipanga vyema kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwemo utekaji.
Aidha RC Chalamila amesema Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za makundi yote ndani ya jamii ikiwemo vijana hivyo ni muhimu kuondoa taharuki kwenye jamii kwani Serikali imepokea changamoto za makundi yote

Vilevile RC Chalamila ametumia Mkutano huo kuwataka wahariri,wanahabari na jamii kwa ujumla kuiamini tume iliuoundwa na Rais Dkt Samia na kusubiri matokeo sahihi yatokanayo na tume hiyo badala ya kila mtu kutoa taarifa akitumia fikra zake akiwa kwenye taharuki huku pia akiitaka jamii kujielekeza kwenye hoja ya maridhiano ili kijua nini kinahitaji kuboreshwa
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Jumanne Muliro amezungumzia majukumu ya jeshi la polisi na uwepo wa mipaka ya kiutendaji kwa kila kundi ili kuimarisha amani na amesisitiza kuwa jishi hilo litaendelea kushirikiana na waandishi wa habari huku akiiasa jamii kutoshabikia vurugu na uvunjifu wa amani

Hata hivyo Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri nchini TEF Deodatus Balile amesema wao kama wahariri wanatambua umuhimu wa uwepo wa amani na wapo tayari kushiriki kikamilifu kudumisha amani ya nchi na kusisitiza uandishi uliojikita kwenye ukweli licha ya uwepo wa viashiria vya uvunjifu wa amani huku mmoja wa wahariri na Mwanahabari mkongwe Absalom Kibanda akisisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kufanya kazi kwa uhalisia na sio kusukumwa na hisia na ushabiki na amesisitiza Jeshi la Polisi kushirikiana na wanahabari wakati wa vurugu
Naye Joyce Shebe ni mmoja wa wahariri waliopata fursa ya kutoa maoni ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kuweka mazingira bora kwa wanahabari kufanya kazi pia wanahabari kufanya kazi za uchunguzi kuhamasisha amani pamoja na kufafanua habari zenye maslahi mapana kwa jamii


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa