Maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji Duniani katika mkoa wa Dar es Salaam yameadhimishwa leo tarehe 22/03/2018 katika viwanja vya Mburahati barafu yakipambwa na matukio muhimu mawili ya Uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi mkubwa wa uchakataji maji taka na upandaji miti kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya ubungo amesema maadhimisho ya wiki hii ya maji kimkoa kilele chake kinaadhimishwa hapa kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa uchakataji maji.
Lakini pia kwa kipindi cha wiki nzima tumekuwa tukishiriki katika shughuli mbalimbali tukikumbushwa namna bora ya kutunza vyanzo vya maji ili mkoa wetu wa Dar es salaam huduma hiyo ya maji ipatikane vizuri na tuwe na maji ya kutosha na salama.
"Kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema hifadhi vyanzo vya maji na mifumo ya ikolojia kwa maendeleo ya jamii" Alisema Kisare.
Mgeni rasmi katika hotuba yake amesema amefurahishwa kusikia katika wiki hii ya maji mkoa umeshiriki katika shughuli za upandaji miti katika chanzo chetu kikuu cha maji ambacho ni mto Ruvu.
Pia utoaji wa semina na elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira ili kuweza kuvilinda vyanzo vyetu viweze kuwa na maji wakati wote yatakayotuwezesha kukidhi mahitaji katika mkoa wetu.
Ujenzi wa mradi huu wa uchakataji maji taka kwa wakazi wa Mburahati utawasaidia kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.
Pia maji yaliyochakatwa yataweza kutumika katika kilimo cha mbogamboga na uzalishaji wa gesi kwa matumizi ya majumbani.
Kwa mkoa wa Dar es Salaam vyanzo vya maji vinavyotegemewa ni mto Ruvu na visima kwa sasa maji yanayopatikana yanakidhi mahitaji ya jamii kwa takribani asilimia 75 hivyo jitihada inafanyika kuweza kufikia asilimia 95 hadi 100 ifikapo mwaka 2025
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Halmashauri zote tano za mkoa wa Dar es Salaam Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na mwenyeji Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa