Zoezi la kutafuta haki ya Watoto waliotelekezwa limekuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya Kinababa 2,008 wamekubali kwa maandishi kutoa Pesa ya Matunzo ya Mtoto huku Watoto 2,971 wakiandikishwa kwa ajili ya kupatiwa Bima ya Afya Bure.
Akitoa tathimini ya zoezi hilo lililohitimishwa leo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amesema tangu kuanza kwa zoezi hilo zaidi ya Wananchi 17,000 walijitokeza kwa ajili ya kupata huduma na Kati ya hao wananchi 7,184 wamesikilizwa huku wananchi 10,000 wakiwa bado hawajasikilizwa na Wananchi 270 wakipimwa DNA.
Kutokana na ukubwa wa tatizo la familia kutotekeleza vyema majukumu yake RC Makonda ameunda Kamati ya Wataalamu 15 wakiwemo Wanasheria, Maafisa Ustawi wa Jamii, Jeshi la Polis Dawati la jinsia na Asasi za kiraia itakayofanya kazi ya kupitia mapungufu ya kisheria na Changamoto zilizojitokeza kisha kutoa mapendekezo kwa ajili ya kufikishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya maboresho ambapo kamati hiyo itaanza kazi May 05 chini ya Mwenyekiti wake Wakili Albert Msando.
Aidha RC Makonda amesema tayari amekabidhi Jeshi la Polisi majina ya kinababa waliokaidi wito wake ambapo kwa wale walioko Mikoani barua zitapelekwa kwa Wakuu wa Mikoa na waliopo Nje ya Nchi majina yatafikishwa kwenye Ofisi za Ubalozi kwa ajili ya utekelezaji.
Hata hivyo RC Makonda amesema kupitia zoezi hilo limefanikisha watoto wawili wenye asili ya China kupata matunzo hadi watakapokuwa wakubwa chini ya jumuiya ya Watu wa China.
Pamoja na hayo RC Makonda amewashukuru wanasheria, maafisa ustawi wa jamii, dawati la jinsia, wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na vyombo vya habari kwa kushirikiana nae bega kwa bega kufanikisha Zoezi hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa