Kilimo ni Sekta muhimu kwa maisha na uchumi wa wakazi wa Mjini na pembezoni mwa Mji.
Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa Mikoa ambayo Kilimo huchangia katika kuongeza kipato kwa wakazi, upatikanaji wa chakula (lishe bora) na hifadhi ya mazingira. Takribani asilimia thelathini (30%) ya mazao ya kilimo yanayotumiwa na wakazi wa Jiji huzalishwa katika maeneo mbalimbali katikati na pembezoni mwa Jiji. Mboga za majani na matunda ni mazao muhimu yanayozalishwa kutokana na kuwa karibu na soko (walaji) na bei nzuri. Mboga zinazozalishwa ni mchicha, matembele, chainizi kabichi, bamia, kisamvu, sukuma wiki, bilinganya, uyoga, mnavu, kisamvu na maboga. Matunda ni pamoja na makakara, matango, papai, nanasi, matikiti maji, na machungwa.
Mkoa una fursa nyingi katika kilimo kutokana na kuwa karibu na soko kubwa (walaji), makampuni ya usindikaji na miundombinu mizuri ya usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi. Mkoa una makampuni makubwa na madogo ya usindikaji wa mazao ya kilimo kama vile matunda, nafaka, na viwanda vya nguo.
Aidha maduka makubwa ya kisasa (shopping malls) yanayoendelea kuongezeka yamekuwa chanzo kingine cha soko la mazao ya kilimo. Mwingiliano wa watu wa mataifa mbalimbali katika mkoa wa Dar es Salaam ni chanzo kingine cha soko la bidhaa mbalimbali za kilimo. Tabia ya ulaji (feeding habit) za watu wa mataifa mbalimbali hutoa wigo mpana kwa wazalishaji kupanua wigo wa mazao kulingana na mahitaji halisi. Katika kupanua wigo wa mazao ya kilimo, Mkoa umeanzisha zao la mchicha nafaka ambao kwa mujibu wa wataalam wa lishe umeonesha kuwa na virutubisho muhimu kwa afya ya mlaji. Mchicha huu huzalishwa kwa wingi kupitia vikundi vya wakulima wa manispaa ya Kinondoni.
Vilevile kadri kipato kinavyoongezeka ndivyo jamii inavyojali ubora wa chakula (food quality) kuliko wingi (food quantity). Takwimu zinaonesha kuwa kaya za jijini Dar es Salaam zina kiwango kidogo cha umaskini wa mahitaji ya msingi ukilinganisha na kaya zinazoishi katika miji mingine na maeneo ya vijijini. Hii ni fursa kwa wazalishaji, wataalam wa ugani, wawekezaji na wadau mbalimbali wa kilimo kuongeza thamani katika bidhaa za kilimo na kuzingatia ubora katika uzalishaji, hususani matumizi ya kilimo hai (organic agriculture) ili kuchangamkia fursa hii inayoongezeka kwa kasi kutokana na kukua kwa kipato na uelewa wa wakazi wa Dar es Salaam.
Mazao kama vile korosho, muhogo na viazi huzalishwa kwa wingi katika Manispaa ya Temeke na Ilala. Usindikaji wa unga wa muhogo na korosho hufanywa kupitia vikundi vilivyopo katika Manispaa za Ilala na Temeke. Uwepo wa Bandari ya Dar es Salaam, barabara zinazokwenda mataifa jirani, Mamlaka za Serikali kama vile Wizara mbalimbali za Kisekta ni fursa ambazo zinaweza kutumiwa na wazalishaji, wasindikaji na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo katika kuzalisha, kusindika na kusafirisha bidhaa za kilimo nje ya nchi na kujipatia fedha za kigeni kwa ustawi wa taifa letu. Aidha uwepo wa taasisi nyingi za fedha, taasisi za utafiti, NGOs zinazojihusisha na kilimo vyote kwa ujumla vinaweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa kilimo mjini (urban agriculture).
Mkoa umetawaliwa kwa kiasi kikubwa na udongo wa kichanga kwa takribani kanda zote za kilimo. Kuna ukanda wa juu ambao umezungukwa na miinuko. Maeneo haya ni yale ya Magharibi na Kaskazini mwa Jiji. Ukanda wa chini umeundwa na mabonde ya Msimbazi, Jangwani, Mtoni, Afrikana, Kimbiji, Kitunda na maeneo ya Ununio na Mbweni .
Eneo linalofaa kwa kilimo na ufugaji ni hekta 107,500, ambapo Manispaa ya Temeke ni hekta 55,000, Kinondoni hekta 37,000 na Ilala hekta 15,000. Hadi sasa eneo linalotumika kwa kilimo ni Ha.32, 972 sawa na asilimia 31 ya eneo lote. Changamoto inayoikumba Sekta ya Kilimo katika mkoa wa Dar es Salaam ni kupungua kwa ardhi ya kilimo kutokana na mashamba kutwaliwa kwa ajili ya viwanja vya makazi na uwekezaji mbalimbali.
Mkoa una masoko makuu ambapo bidhaa mbalimbali za kilimo hupatikana. Masoko hayo yanapatikana katika Halmashuri tatu za Manispaa (Ilala, Kinondoni, Temeke Ubungo na Kigamboni).
Changamoto dhidi ya kilimo ni kupanuka kwa kasi kwa Jiji hivyo maeneo mengi ya kilimo kufanywa makazi ya watu na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii. Hii ni fursa pia kwa uzalishaji wa mazao yenye thamani (high value crops) na matumizi ya teknolojia zinazohitaji eneo dogo la ardhi kama vile "green houses" ili kufanikisha kilimo-biashara mjini. Aidha kumekuwa na uharibifu mkubwa wa bidhaa sokoni (post harvest loss) kutokana na miundombinu mibovu ya masoko na ukosefu wa maghala ya kisasa. Hii ni fursa kwa wawekezaji kuanza kufikiria kuwekeza katika miundombinu kama vile "cold rooms" na maghala ya kisasa (silos) ili kupunguza uharibifu ambao umekuwa ukiathiri hali ya usalama wa chakula katika Jiji la Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa