Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul C. Makonda amefanya ziara ya kutembelea Miradi Mikubwa inayotekelezwa na Serikali na kusimamiwa na DAWASA tarehe 08/06/2017 kwa lengo la kujionea kazi kubwa inayofanywa na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Awali Mhe. Paul Makonda akiwa katika Ofisi ya DAWASA Makao Makuu alipokea taarifa kutoka kwa Maafisa Watendaji wakuu wa DAWASA na DAWASCO kuhusu uwepo wa taasisi hizo, majukumu yao, mafanikio na changamoto zilizopo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa baada ya kupokea taarifa hizo alianza ziara ya kutembelea miradi hiyo ambapo alianza kwa kujionea mradi wa Tangi la Maji maeneo ya Kibamba na kupata maelezo ya mradi huo halafu akaelekea katika mradi wa Ruvu juu Darajani ambapo hapo alijionea mitambo ya uzalishaji wa maji sambamba na kukagua kituo kipya cha kusukuma Majighafi na kupata maelezo ya uendeshaji wa kituo hicho.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alitembelea pia Mradi wa Maji Ruvu Juu na kukagua Mitambo Mipya ya kutibu maji na Kupata maelezo ya uendeshwaji wa mitambo hiyo, halikadhalika alimalizia kwa kutembelea Mitambo mipya ya usafishaji,kutibu na kusukuma Maji ya Ruvu Chini na kukagua mitambo hiyo ikiwemo kupata maelezo ya upanuzi wa Mitambo hiyo.
Baada ya hapo Mhe. Paul Makonda alipata nafasi ya kuongea ambapo alisema kuwa amefurahishwa sana na juhudi kubwa zinazofanywa na watendaji wa Sekta hiyo ya Maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa nafasi ya kipekee alimshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwajibikaji wake na kuwateua watu wanaoweza kufanya kazi kikamilifu akiwemo Waziri wa Maji, Katibu Mkuu wake na Hatimae kutupatia DAWASA na ikapelekea kupatikana kwa DAWASCO ili kuhakikisha watu wanapata majisafi.
Mhe. Paul Makonda amesema kuwa kwa upande wa Ruvu juu wameongeza uzalishaji wa maji kwa kiwango cha lita Millioni 196 zinazozalishwa kwa siku aidha Ruvu chini ambapo nao wanazalisha zaidi ya lita Millioni 270 ambapo yakijumlishwa haya maji ni mengi sana na kupelekea kupunguza kero ya maji katika Jiji letu la Dar es Salaam. Aidha, mkakati wa kuendelea kupunguza maji yanayopotea ni mkubwa. Wakati huo huo mfumo wa maji taka unaendelea kuudhibitiwa ili kuondoa kabisa tatizo la mfumo huo unaosababisha magongwa mbalimbali.
Mhe. Paul Makonda aliwataka wananchi wote wasiokuwa na huduma ya maji katika maeneo yao kufika katika Ofisi za DAWASCO kujisajili ili kuwekewa miundombinu ya maji na kisha kupata maji na kuwekewa utaratibu mzuri wa kuyalipia maji hayo kupitia Ankara zao
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Injinia Romanus Mwang’ingo alieleza kuwa wamempitisha Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Miradi inayotekelezwa na kusimamiwa na DAWASA ili kuona hali halisi na anaamini kuwa ndani ya mwaka mmoja ujao kwa wale waliokuwa hawana maji watapata maji na wale waliokuwa hawana mtandao wa maji pia wataupata kwani mkandarasi wa kusambaza maji yupo kazini.
Vile vile Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Injinia Cyprian Luhemeje alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda namsafara wake kwa kuwatembelea na kujionea hali halisi sambamba na kueleza kuwa mpango mkakati umewekwa wa kuhakikisha ndani ya mwaka mmoja watafika asilimia 85 na pamoja na kupunguza ya usambazaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa