Waziri wa ujenzi Mhe Innocent Bashungwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila leo Novemba 14, 2023 wameendelea na ziara na kukagua miradi ya barabara Chanika-Msongola mpaka Mbande
Wakiwasili eneo la Msumbiji, Chanika walikuta jinsi wafanyabiashara walivyopanga bidhaa zao karibu na barabara huku wengine walivyojenga kwenye hifadhi za barabara na kusababisha magari kupita kwa shida hali inayopelekea kuwe na foleni.
Mhe. Bashungwa aliwataka wananchi wa eneo hilo kujiandaa kisaikolojia kuhama katika eneo hilo kupisha ujenzi wa barabara na 'round about' ya kisasa kwasababu wapo ndani ya hifadhi ya barabara na hakuna sheria inayomruhusu yoyote ndani ya mita 22.5 kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1932 hata kama wamepeleka zuio hilo mahakamani.
Akiwa eneo la Msongola Mhe Waziri alikagua barabara ya Msongola-Mbande na kujionea jinsi mkandarasi aliyekabidhiwa ujenzi huo akifanya uzembe kwa kisingizio cha mvua na kuchelewesha mradi huo na kupewa mwezi mmoja barabara hiyo iwe imekamilika yenye urefu wa KM 3.8.
Vilevile Mhe. Bashungwa aliwasihi wakandarasi wazawa watumie fursa wanazozipata ili wajitengenezee sifa nzuri, "Ninatoa wito kwa wakandarasi wazawa msitie aibu kama hii tuliyoiona hapa. Wananchi wanapokuona umechukua muda mrefu wanaona ni mbabaishaji."
Mhe Chalamila naye aliongezea, "Nikiri kwanza mkandarasi huyu ana bahati sana nilikuwa sijafika kabla yako Mhe Waziri. Sababu za mvua zipo, vilevile na wengine wameshamaliza miradi hii na mvua ipo, huyu bwana alipaswa kuchukuliwa hatua, na hatua kubwa yakuchukuliwa ni kulala ndani kwanza."
Pia RC Chalamila aliongea na wananchi hao kutokana na changamoto wanazopitia wataandaa mkutano na mkuu wa wilaya Jumatatu ijayo kuanzia saa 6 mchana mpaka saa 12 jioni kuweza kusikiliza kero wanazopitia zikiwemo athari za mvua zinazoendelea, migogoro ya ardhi na viongozi wala rushwa.
Akitoa salamu kutoka kwa Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan Mkuu wa Mkoa aliwambia wananchi kuwa kutakuwa na awamu nyingine ya kujenga barabara za mwendo kasi ili kuondoa adha ya usafiri sababu upande ule una wananchi wengi, na kuwapa pole wote waliokumbwa na mafuriko
Wananchi nao walioeleza kero wanazozipa zikiwemo kukosa mifereji, vituo vya daladala, matuta na alama za barabarani, na kulaumu mkandarasi kushughulika na barabara akiona viongozi, huku wengine wakiomba barabara zinazopita ndani ya mitaa zifukiwe kutokana na kuharibiwa na mvua za El-Nino zinazoendelea kunyesha
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa