-Serikali yatoa ahadi kufanya kila linalowezekana barabara zipitike, mvua zikiisha ujenzi utaanza rasmi
Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila na wataalam wengine leo April 29, 2024 amefanya ziara katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua katika Wilaya ya Kigamboni na baadae kukagua eneo la Kivuko Magogoni
Mhe Waziri alianza ziara yake katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo alipatiwa taarifa fupi ya athari ya mvua katika Mkoa huo kutoka kwa mwenyeji wake Mh Albert Chalamila na Meneja wa TANROAD mkoa huo.
Akiwa katika barabara ya kibada-mwasonga Waziri Bashungwa amekagua barabara hiyo ambayo imeharibiwa na mvua ambapo ametoa kauli ya Serikali kuwa tayari mkandarasi ameshapatikana barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami urefu wa Km 51 "wananchi wawe na subra Serikali kwa sasa inafanya ukarabati wa kawaida kurejesha mawasiliano lakini mvua zikiisha tu ujenzi utaanza rasmi" Alisema Waziri Bashungwa
Aidha akiwa katika barabara ya Kigamboni-mwasonga eneo la Magogoni alipata wasaa wa kukagua barabara hiyo na kuongea na wananchi ambapo amewahakikishia kuwa kutakuwa na timu maalum ya kufanya tathimini ya uharibifu wa miundombinu katika Mkoa huu ambayo itaripoti katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ikimaliza tathimini yake maeneo yote yenye changamoto yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amesema ukichunguza kwa umakini maeneo yenye mafuriko utaona nyumba zimejengwa katika mikondo ya maji hivyo kuzuia maji kupita ambapo amewataka wataalam kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo ambayo njia za asili za maji zimezibwa ili ikilazimu kama kuna Kuta zibomolewe.
Vile vile Waziri Bashungwa amekagua Kivuko eneo la Magogoni kujionea Changamoto za kivuko hicho na kesho anatarajia kuendelea na ziara yake ikiwa ni siku ya pili katika Mkoa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa