Watendaji wa Ardhi wa Manispaa za Jiji la Dar es salaam leo wamejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupata kigugumizi na kushindwa kujibu maswali ya msingi yaliyokuwa yakiulizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda kuhusu idadi ya Migogoro ya Ardhi katika idara wanazoongoza na kusababisha baadhi yao kudondoka kwa kuzimia na kukimbizwa hospital.
Kitendo cha wakuu hao wa idara kushindwa kujibu maswali ambayo yamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi isiyoisha kimewakera Maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kwaajili ya kujua hatma ya Malalamiko yao na kujikuta wakuomba RC Makonda kuwatumbua.
Kutokana na watendaji hao kushindwa kutekeleza majukumu yao RC Makonda ameagiza wakuu wa idara ya ardhi Manispaa za Ubungo na Ilala wapangiwe kazi nyingine kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Aidha RC Makonda amesimamisha shughuli zote za Mabaraza ya Kata Dar es salaam kuwakuwa hazina uwezo wa kusikiliza kesi na pia hawana wataalamu wa sheria kitendo kinachochangia Migogoro mingi ya Ardhi.
Kutokana na hilo RC Makonda amewataka Makatibu Tarafa kuanza kutembelea Mabaraza hayo kuanzia Jumatatu ya February 12.
RC Makonda amechukuwa uamuzi huo wakati wa kupokea Ripoti ya Malalamiko ya Wananchi waliodhulumiwa Haki zao ambapo zaidi ya Wananchi 11,652 walifika kwaajili ya kupata Msaada wa kisheria ambapo jumla ya malalamiko 3,373 yalipokelewa na kusikilizwa huku wananchi waliosikilizwa wakiwa ni 6,052 na ambao hawakupata fursa ya kusikilizwa wakiwa ni Wananchi 5600 ambapo leo RC Makonda ameandaa utaratibu wa kuhakikisha wote wanasikilizwa.
RC Makonda amesema idadi kubwa ya wananchi waliokimbilia kwake kutafuta haki ni tafsiri tosha kuwa baadhi ya watendaji hawasimami ipasavyo katika nafasi zao ambapo amewaagiza Wakurugenzi kuanza kupitia wasifu wa wakuu wa idara CV na kazi zote wanazofanya.
Ili kuhakikisha wanyonge walioporwa haki zao wanazipata pasipo kuvunja sheria RC Makonda amewasilisha kwa Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam Majina ya watu wenye michezo ya kudhulumu wananchi kwaajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Makonda ameagiza Watendaji kuhakikisha malalamiko yote ya wananchi ya Migogoro ya ardhi, Mirathi,Talaka, Madai, Makosa ya jinai, Masuala ya kazi, Ubakaji na utapeli yanafanyiwa kazi kabla ya mwezi April.
Aidha amewataka madalali wote wanaofanya kazi ya kutekeleza hukumu za Mahakama au Bank kufika ofisini kwake siku ya jumanne wakiwa na nyaraka za usajili.
Nao baadhi ya Wananchi waliofika kwenye mkutano huo wamefurahia hatua za RC Makonda katika kuwajali wananchi wanyonge ambapo pia wameshukuru mkutano huo umewasaidia kujua kwa undani masuala ya kisheria.
Aidha wamesema kuwa wanaamini kwa ujasiri RC Makonda wanafarijika kuona tabu waliyoipata kwa miaka mingi wakitafuta haki yao inaenda kupatikana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa