- Asema magonjwa yasiyoambukiza yanameongeza vifo zaidi 26% ya vifo vyote Nchini
- Abainisha wengi wa waathirika ni kuanzia miaka 35 na Chini ya miaka 60 tofauti na zamani ilikuwa ni watu wazima/wazee
- Aelekeza kila Wilaya ndani ya Mkoa kuhamasisha Wananchi kujikinga na Magonjwa yasiyoambukiza
- Asema Mkoa umeandaa KADI MAALUM itakazomuwezesha mwananchi kufuatilia AFYA yake
- Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza DSM Dkt Digna Riwa afafanua KADI hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makalla leo Novemba 3, 2021 amewataka wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujikinga na Magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mitindo ya Maisha.
Mhe Makalla ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano Arnatoglo-Ilala Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kiasi kwamba yameongeza vifo kwa zaidi ya 26% ya vifo vyote Nchini hivyo kupitia wiki ya Maadhimisho ya magonjwa yasiyoambukiza wananchi inayoanza *Novemba 06, hadi 13, 2021, WAJITOKEZE kupima na kupata ushauri wa Kitaalam* ili waweze kubadili mitindo ya Maisha
Mhe Makalla amefafanua waathirika wengi siku hizi ni kuanzia umri wa miaka 35 na Chini ya miaka 60 tofauti na ilivyokuwa zamani magonjwa hayo yalikuwa yanawapata wazee/watu wazima zaidi ya miaka 60.
Aidha kupitia kauli mbiu ya mwaka huu Badili Mtindo wa Maisha " ameelekeza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kusimamia zoezi hilo na kuhamasisha Wananchi katika maeneo yao katika Maadhimisho ya wiki ya magojwa yasiyoambukiza.
Sambamba na hilo Mkoa umeandaa KADI MAALUM zitakazogawiwa katika Wilaya zote za Mkoa ambazo zitamuwezesha mwananchi kufuatilia mwenendo wa Afya yake na badaye kumuona mtaalam husika, kama ni lishe atamuona mtaalam huyo.
Akifafanua KADI hiyo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Tiba, na mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Digna Riwa amesema kupitia kadi hiyo itakuwa ni rahisi kufuatilia mwenendo wa afya mara baada ya kupima na kuweza kujua majibu ya afya yako kwa kuwa KADI hiyo inaelekeza kila hatua na nini cha kufanya.
"Mtu yeyote atakuwa na uwezo wa kufuatilia AFYA yake mahali popote hata kama hakuna mtaalam wa afya" Alisema Dkt Digna
Ifahamike kuwa Maadhimisho hayo ya wiki ya magojwa yasiyoambukiza* katika Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam yataambatana kufanya Mazoezi ya Kukimbia " Jogging" pia kupima na kupatiwa ushauri wa Kitaalam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa