Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Amos Makalla akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makalla ametoa tamko hilo leo ofisini kwake wakati anaongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa “UVIKO -19” kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe Mkuu wa Mkoa amezitaka kamati zote za ulinzi na usalama katika wilaya za Mkoa kusimamia katika maeneo yao utekelezaji wa mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto katika kukabiliana na wimbi la tatu la kuenea kwa ugonjwa wa KORONA au UVIKO-19.
“Kuanzia leo wananchi wavae barakoa katika maeneo mbalimbali iwe ni kwenye Daladala, Mwendokasi na vyombo vingine vya usafiri, aidha vyombo vya umma vya usafiri kuwe na “level seat” vilevile maeneo yote ya mikusanyiko iwe kwenye sherehe, matamasha, kwenye ibada na hata maofisini viwepo vifaa vya maji tiririka na vitakasa mikono” Alisema RC Makalla
Sambamba na hilo Mhe Mkuu wa Mkoa amesema shughuli zote za kiuchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam ziendelee kama kawaida lakini taadhari dhidi ya KORONA au UVIKO – 19 zichukuliwe tena kwa umakini mkubwa kwa kuwa ugonjwa huo upo nchini.
Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imejipanga vizuri kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika kukabiliana na ugonjwa huo, tayari ofisi yake ilishafanya ziara katika vituo vya afya na Hospitali za Mkoa kujiridhisha uwepo wa vifaa vya kuweza kutoa huduma pale wagonjwa wakibainika.
Msisitizo wa mkuu wa Mkoa kwa wananchi wote ndani ya Mkoa ni kusitisha mikusnyiko isiyokuwa ya lazima, katika maeneo ya Stendi za mabasi, daladala, bodaboda kuzingatia ukaaji wa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu, kunawa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na uvaaji wa barakoa.
Mwisho jukumu la Mkoa sasa ni kufanya ziara za kushitukiza kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam kuona utekelezaji wa mwongozo huo wa udhibiti wa ugonjwa wa KORONA kupitia afua ya kudhibiti misongamano katika jamii bila kuathili shughuli za kiuchumi na ofisi ya Mkoa ipo tayari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA HABARI NA UHUSIANO
MKOA WA DAR ES SAALAM.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa