Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na WHO imegawa jumla ya Apron 257 zenye thamani ya Tshs 2,929,800/= kwa Mama lishe na Baba lishe wa Soko la Buguruni – Ilala na Sterlio – Temeke leo asubuhi kufuatia juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali ya Mkoa katika kupambana na ugonjwa hatari wa kipindupindu.
Zoezi hilo la ugawaji wa Apron lilipokelewa vema katika Masoko yote kwa wahusika kujitokeza kwa wingi ili waweze kupokea Apron zao kwa ajili ya kudumisha usafi katika maeneo yao ya kazi.
Awali Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Dennis Kamzolah aliwaambia Mama lishe na Baba lishe wa Soko la Buguruni kuwa maeneo yao yanapaswa kuwa masafi kwani kinyume chake ugonjwa hatari wa kipindupindu utatokea na ukitokea utasababisha vifo vya watu sambamba na kufunga biashara hivyo itakuwa hasara pia kwa upande wao.Aliwataka kuweka chakula chao katika mazingira safi na salama. Aidha, kuwawekea misingi ya usafi wateja wao pindi wanapokuja kwa kunawa katika maji ya moto na sabuni, kuwa na kapeti la kuwekea vyombo, Dustibins n.k.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buguruni Bw. Adam Fugame aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na WHO kwa kugawa Apron hizo kwa Mama lishe na Baba Lishe wa soko lake na kuwataka kina Mama lishe na Baba lishe kuzingatia yote wanayopaswa kuyazingatia ili kuepukana na magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na uchafu.
Katika Soko la Sterlio – Temeke Kaimu Afisa Afya wa Manispaa ya Temeke Bi. Rehema S. Ally aliwaeleza Mama lishe na Baba lishe waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kupewa Apron kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao msingi mkubwa ni Usafi kwani bila kuzingatia hilo itapelekea kutokea kwa magonjwa mbalimbali katika biashara zao. Hivyo aliwataka kuzingatia kanuni zote za Afya.
Akitoa shukrani kwa Serikali ya Mkoa na WHO Baba lishe Bw. Mussa D. Jumbe amesema wamepokea Apron kwa furaha na wanaamini itakuwa ni chachu kwao kwa ajili ya kuwahamasisha wazidi kuzingatia suala la usafi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa