Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kampuni ya Wastewater Solutions imepanga mkakati wa kudhibiti maji taka yanayotiririshwa ovyo Jijini Dar es Salaam na kusababisha madhara mbalimbali kama vile uhalibifu wa Mazingira, uchafu, mmomonyoko wa udongo, upotevu wa viumbe mbalimbali ardhini na milipuko ya magonjwa mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Dennis Kamzola alipokuwa akifungua mkutano wa Kuitambulisha Oswams kwa wadau wa Mazingira waliohudhuria katika Mkutano huo.
Amesema kwa sasa mifereji inayopitisha maji machafu na maji ya mvua imeanza kukarabatiwa, kutoa elimu ya Afya kwa wananchi na uwepo wa tozo za papo kwa papo kwa wote wanaokiuka taratibu zilizowekwa za kutunza Mazingira. Aidha, Maafisa Afya wameendelea kusisitizwa kuzingatia sheria ya Afya na usafishaji ya mwaka 2009
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Mkoa wa Dar es Salaam Dr Churchill Mjuni amesema mbali na hayo Mkoa umejipanga katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kujenga mifereji ya asili eneo la Bungoni Malapa na Mtoni kwa Azizi Ally vilevile kujenga ukuta wa kuzuia kuongezeka kwa maji ya Bahari kwenye barabara ya Barack Obama na kujenga ukuta wa kuzuia maji ya Bahari katika Chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni, Kugawa majiko banifu 4500 ya mkaa kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa ili kupunguza matumizi ya mkaa na ukataji miti ovyo, Kupanda mikoko, Kuboresha bonde la mto Msimbazi kwa kulifanya kuwa la kitalii zaidi, kuwatumia Wadau wa ramani huria kutambua kata zote ambazo ziko kwenye hatari ya kupata mafuriko ili kuwajengea uwezo watu hao wa namna ya kukabiliana nayo pindi yatakapotokea.
Kwa upande wake Mhandisi Juma M. Nassor mtaalamu wa ufundi kutoka kampuni ya Wastewater Solutions amesema kati ya asilimia 80 ya majitaka yanayozalishwa ni asilimia 10 tu ndio hutibiwa kwa kuwa mifumo iliyojengwa ili kusafirishia maji hayo kutoka majumbani au viwandani kwa sasa haina uwezo tena jambo ambalo linasababisha maji hayo kufurika na kusababisha magonjwa ya mlipuko, na kwamba wamejipanga kulidhibiti hilo kwa kuzalisha majitaka ambayo yamekidhi viwango visivyoharibu mazingira kwa kutumia mitambo na njia za kisasa zaidi.
Hata hivyo ameongeza kuwa kukamilika kwa mpango huo kutawezesha kugeuza majitaka hayo kuwa katika matumizi salama, upatikanaji wa nishati ya gesi (Bio gas), upatikanaji wa mbolea, pia maji hayo yatatumika katika umwagiliaji wa bustani sambasamba na kusaidia kupunguza kama sio kumaliza tatizo la magonjwa ya mlipuko.
Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Idara ya Afya Bw. Salvata Silayo, ameitaka kampuni hiyo kuwa na wataalamu wa kutosha ili kuhakikisha wanapata vibali vyote stahiki sambamba na kuhakikisha wafanyakazi wanapata vifaa kinga ili kuwaepusha na Magonjwa .
Aidha, Mratibu wa Mazingira kutoka NEMC Bw. Jaffar Chimgege amewataka wananchi wa Dar es Salaam kuchangamkia fursa ya OSWAMS ili kutibu maji taka katika mazingira yao. Amesema hii inasaidia kupunguza au kuondoka tatizo la utupaji wa maji taka kwani ni makosa hivyo yakitibiwa yatatumika tena kama rasilimali.
Akifunga mkutano huo Afisa Afya wa Mkoa amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo sambamba na kuwaomba wadau mbalimbali wa Maendeleo kuendelea kujitokeza ili kuchangia katika sehemu mbalimbali ili kulifanya Jiji letu kuwa sehemu safi na salama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa