Ubalozi wa China Nchini Tanzania umeguswa na kazi nzuri inayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ya kuboresha mazingira ya walimu na kuamua kumzawadia Majengo Matano ya kisasa kwa ajili ya ofisi za walimu ambapo leo RC Makonda ameweka jiwe la Msingi kuashiria kuanza kwa Ujenzi huo kwenye Shule ya Sekondari Makumbusho pamoja na kukabidhi Ramani ya Majengo.
Ujenzi wa Majengo hayo Matano ni matokeo ya RC Makonda kuwasilisha ombi la ujenzi wa ofisi za walimu kwa Balozi wa China nchini Tanzania na kwa kuwa kazi anayofanya RC Makonda inaonekana Balozi huyo alipokea kwa mikono miwili ombi hilo.
Majengo hayo yatajengwa kwenye Wilaya Tano za Mkoa wa Dar es salaam ambapo ndani yake zitakuwa na Ofisi ya Mwalimu Mkuu, Mwalimu mkuu msaidizi, Ofisi ya walimu wote, ukumbi wa mikutano, chumba cha kuhifadhi mitihani, vifaa vya michezo, chumba cha muhasibu, chumba cha kubadili nguo, mapokezi, vyoo, bafu huku zikisheheni furniture za kutosha ikiwemo viti, meza, makabati na AC ambapo ujenzi wa jengo hilo unataraji kukamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
RC Makonda amemshukuru Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke kwa ujenzi wa majengo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaenda kupunguza mateso ya walimu kufanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo kufanya kazi kwenye madarasa.
Amesema dhamira yake katika kuboresha mazingira ya walimu ni kuwawezesha kutoa elimu bora itakayowezesha Taifa kuwa na wataalamu wa kutosha.
Kwa upande wake Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke amesema kwa miezi mitatu aliyoishi hapa nchini tangu alipoteuliwa kuwa balozi ameshuhudia maendeleo makubwa aliyofanya RC Makonda hivyo wameona wasikae kimya kwenye jambo hilo linalolenga kuleta ukombozi wa uchumi kupitia elimu.
Nao walimu wa shule ya makumbusho wamemueleza RC Makonda kuwa awali walikuwa wakitumia madarasa manne ya wanafunzi hivyo ujenzi wa jengo hilo ni neema kwao kwa kuwa madarasa hayo yatarejeshwa kwa wanafunzi.
TUSHIRIKIANE KWA PAMOJA KUBORESHA MAZINGIRA YA ELIMU KWA MANUFAA WATOTO WETU.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa