Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Felix Lyaniva amewaongoza wafanya kazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda kwa kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyoadhimishwa katika Uwanja wa Uhuru jijini hapo.
Awali Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Temeke alipokea maandamano ya wafanyakazi hao yaliyoanzia katika Jengo la TUCTA Mnazi Mmoja na kupita mbele yake yakiwa na jumbe mbalimbali.
Akizungumza katika maadhimisho hayo DC Lyaniva amewataka Waajiri wote katika Mkoa huo kufuata Sheria ya Ajira ya kuwapatia wafanyakazi mkataba na kudumisha Usalama wa Kazi.
Amesema wapo baadhi ya Waajiri ambao hawatoi Mkataba wa kazi na badala yake wanashikilia vyeti vya wafanyakazi hao jambo linalopelekea Waajiriwa kufanya kazi katika mazingira magumu.
"Niagize kila Mwajiri ahakikishe uwepo wa mkataba wa ajira na Usalama kazini ili kuboresha mazingira ya wafanyakazi wao kwani wasipokuwa na mkataba haki zao hawatazipa kama inavyotakiwa”.
Aidha amewataka Maafisa kazi kuhakikisha wanasimamia haki na stahili za wafanyakazi ili kutengeneza mazingira mazuri ya kazi.
Pia amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kwa haki na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea katika kuwahudumia wananchi bila kudai rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na maendeleo kwa ujumla.
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma bora na kuwathamini wafanyakazi na kuhakikisha Sekta za Umma na Binafsi zinatatua kero mbalimbali za wafanyakazi.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema, Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Theresia Mmbando, Wakurugenzi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Makatibu Tawala wa Wilaya , Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini pamoja na Vyama mbalimbali vya wafanyakazi.
Maadhimisho ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Uunganishaji wa Mifuko ya Jamii Ulenge Kuboresha Mafao ya Mfanyakazi”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa