Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda ameanza kutekeleza AHADI aliyoitoa baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alipofanya mkutano na wenyeviti wa serikali za mitaa kuhusu Kupanga Mji katika muonekano mzuri wa jiji la biashara utakaovutia wananchi wengi wa ndani na nje kuja kufanya biashara Dar es Salaam kwa kuzindua mpango mkakati wa Ujenzi wa Eneo Moja kubwa la kufanyia biashara ya kuuza magari (used cars) pamoja na vifaa vya magari na huduma zingine zinazoendana na Biashara hiyo ikiwemo Utoaji wa bima na lesesni za magari, Huduma za kibenki, Ofisi za mamlaka ya Mapato (TRA) katika eneo moja (one car stop center) katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe Paul Makonda amesema tayari Serikali ya Mkoa imeshatenga eneo kubwa na la kutosha katika Manisapaa ya Kigamboni ambalo litatumiwa na wafanyabiashara wote wa magari katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo katika utekekezaji wa mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda ametoa "OFFER" ya Bure kwa miaka mitatu kwa wafanyabiashara kutumia eneo hilo pasipo Malipo au tozo ya Kodi ya Pango au Kiwanja hatua itakayowawezesha kutumia unafuu huo kujenga uzio na Sehemu za Ofisi katika maeneo hayo, ambapo apo awali wafanyabiashara hao hulazimika kulipa zaidi ya Shilingi milioni Sita kwa ajili ya gharama za kupangisha eneo la kufanya biashara, ambapo kwa sasa watakaa Bure kwa Miezi 36 pasipo kulipa Gharama za Pango
Mhe Paul Makonda amesema azma ya serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ni kutengeneza mazingira mazuri yatakayovutia wawekezaji kuwekeza ambapo katika hatua za awali tayari wafanyabiashara wameonyesha nia ya Kujenga (show room) kubwa za kuuzia magari ambazo zitatumika kuuza magari mpaka yatakayouzwa nje ya nchi, na ndani ya Tanzania.
Mkakati huu pia unalenga kudhibiti vitendo viovu na ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ya magari wasiowaaminifu ambapo katika mpango huu, mteja atapata fursa ya kufika kwenye eneo moja na kuchagua gari analotaka, na kisha kulipia fedha, na kodi ya serikali, na leseni, pamoja na Bima katika eneo moja hatua ambayo itaongeza ukusanyaji wa Mapato ya serikali na kudhibiti Madalali ambao wamekuwa wakipandisha gharama za uuzaji wa magari kwa maslahi yao binafsi.
Utaratibu huu utakuwa ni wa kwanza kuwahi kutekelezwa katika nchi za ukanda wa Africa mashariki, ambao unafanana na utaratibu wa kuuza Magari unaotumiwa katika majiji ya Tokyo Japan, na Dubai nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo kuanzia Leo tarehe 11/09/2017 maeneo yataanza kutolewa BURE kwa wafanyabiashara wote wenye Show room za Magari jijini na baada ya Miaka mitatu Wanaotaka kununua watanunua, na wanaotaka kuendelea kupangisha watapangisha, zoezi hili litahitimishwa mwezi January 2018 ambapo anaamini Show room zote zinakuwa zimehamia Kigamboni, na hakutakiwa tena kuwa na uuzaji wa Magari kiholela katika Mkoa wa Dar es Salaam zaidi ya Kigamboni.
Mhe Makonda amehitimisha kwa kusema mpango huu unaendana na utekekezaji wa AGIZO la Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuwataka Wakuu wa Mikoa kuainisha maeneo ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa ndani na nje yatakayovutia wananchi kuwekeza nakurahisisha utoaji wa huduma bora kwa Wananchi, na kusititiza kuwa Mpango huo utachochea ushindani halali wa biashara ya Magari, ushindani ambao mwisho wa siku utatoa huduma bora kwa Wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa