- Zaidi ya madumu elfu 11 ya mafuta ya kupikia yakamatwa Mbweni
- RC Chalamila aagiza Jeshi la polisi na TAKUKURU kuwahoji kwa kina watumishi wa Bandari ndogo Mbweni
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Februari 21, 2024 ameueleza umma kupitia vyombo vya habari kukamatwa kwa shehena ya bidhaa za magendo, madumu ya mafuta ya kupikia zaidi ya elfu 11 Mbweni
RC Chalamila amesema Kushamiri kwa magendo ni kiashiria tosha kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma wanaohusika hivyo ameagiza Jeshi la polisi na TAKUKURU bila kupapasa macho kuwakamata mara moja watumishi wote wa bandari ndogo ya Mbweni wahojiwe kwa kina ili ukweli ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe.
Aidha RC Chalamila amepongeza kazi nzuri inayofanywa na kikosi kazi katika ukanda mzima wa fukwe ya bahari ya hindi ambapo amesema kikosi kazi hicho kimejipanga vizuri kudhibiti biashara hizo za magendo ambazo zinatoka Zanzibar kuja Tanzania bara ." Hatuwezi kuruhusu bidhaa za magendo kupenya katika Mkoa huu kwa kuwa ni hatari kwa usalama wa watu na Taifa kwa Ujumla" amesistiza Chalamila
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Saad Mtambule amesema kati ya shehena za madumu ya mafuta zaidi ya elfu 11 madumu elfu 3 tu yalikuwa yamelipiwa mengine yote vibali vyake havikuonekana ndio maana yameshikiliwa na kuhifadhiwa katika Bandari kavu ya Ubungo
Ifahamike kuwa shehena hiyo ya mafuta ya kupikia imekamatwa usiku wa kuamkia Februari 21,2024 kupitia juhudi kubwa inayofanywa na kikosi kazi ambapo RC Chalamila ameelekeza kuendeleza mapambano dhidi ya biashara hiyo ya magendo kwa kutumia mbinu za kisayansi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa