Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amesema kinamama wote waliofika ofisini kwake wakiwa na watoto kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kisheria baada ya kutelekezwa atawapatia kadi za Bima ya Afya (Toto Afya Card) Bure kwa ajili ya matibabu ya watoto wao.
RC Makonda amesema kadi hizo zitatolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 17 kwa kila mama aliyefika ofisini kwake pasipokujali idadi ya watoto alionao ambapo katika Zoezi zima zaidi ya watoto 5,000 watapatiwa Bima ya Afya.
Uamuzi huo umekuja baada ya RC Makonda kujionea mateso wanayopata kinamama hao ikiwemo watoto kuugua Magonjwa yanayohitaji gharama kubwa za matibabu na kwa kuwa wengi wa kinamama hao wana hali ngumu kimaisha wanashindwa kumudu gharama na kusababisha maumivu na mateso kwa mtoto.
Aidha RC Makonda amesema hadi kufikia jana zaidi ya kinamama 1,030 walikuwa tayari wamesikilizwa na Kati ya hao watu mashuhuri 107 wakiwemo wanasiasa na viongozi wa dini wametuhumiwa kutelekeza watoto.
Hata hivyo RC Makonda amesema kuanzia wiki ijayo kinababa waliotelekeza watoto wataitwa ofisini kwake kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na atakayekaidi kufika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa