Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda amezindua Jengo la upasuaji na wodi ya wajawazito katika Hospitali ya Mwananyamala lililofadhiliwa na Kampuni ya GSM ambalo limegharimu takribani milioni 420 hadi kukamilika kwake.
Uzinduzi wa jengo hilo umefanyika leo katika Hospital ya Mwananyamala katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya pamoja na viongozi wa vyama na Serikali .
Akizindua jengo hilo leo Mh Makonda amesema jingo hilo litakuwa maalumu kwa ajili ya utoaji wa huduma za upasuaji kwa wajawazito na wagonjwa wengine wa dharura.
"Nitumie fursa hii kuwapongeza GSM foundation kwa support yao kubwa waliyoifanya na kukamilisha ndoto hii ya Muda mrefu ya kupunguza tatizo kubwa la kinamama kugombania chumba kimoja cha operesheni na kusababisha vifo vingi kwa kinamama na watoto " Amebainisha Makonda.
Amesema ujenzi wa jengo hilo pamoja na vitu vingine ni katika kuunga mkono juhudi za Mh Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli katika kuhakikisha huduma ya Afya inaboreshwa hasa ile ya uzazi kwa kinamama na kupunguza vifo vya mama na mtoto kunakosababishwa na kukosa huduma madhubuti kunakoenda sambasamba na mazingira yasiyo rafiki.
Aidha amebainisha kuwa jengo hilo lina vyumba viwili maalum kwa ajili ya upasuaji, vyumba kwa ajili ya uangalizi maalumu, (ICU), vyumba vya uangalizi baada ya upasuaji, vyumba vya utawala pamoja na huduma nyingine.
Kadhalika ameeleza uwezo wa jengo hilo la upasuaji kuweza kupumzisha wagonjwa kumi ambao wamekwisha fanyiwa upasuaji kwa wakati mmoja bila bugudha yoyote, na kufanya upasuaji kwa wagonjwa wawili kwa wakati mmoja.
Naye Maneja Mkuu wa Kampuni ya GSM Eng Hersi Said amesema kwa kampuni yao kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za Afya ni faraja kubwa, na pia ni katika kuhakikisha vifo vya mama na mtoto katika uzazi vinapungua.
Katika hatua nyingine RC Makonda amewataka wananchi wa Mkoa wa Dar És Salaam kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kuweza kupata huduma ya matibabu kwa haraka na kwa wakati.
Pia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Tiba kwa Kadi kutakakomrahisishia mgonjwa kupata huduma kwa haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa