Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amekutana na Mabenki, Wenyeviti wa mitaa, madalali wa mahakama na mabenki kuweka mkakati madhubuti wa kudhibiti wizi na utapeli ambao umekuwa chanzo cha maumivu kwa wananchi.
Katika kikao hicho RC Makonda amewataka watu wa Benki kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kujiridhisha kabla ya kutoa mkopo baada ya kuibuka kwa utapeli wa watu kutumia hati za watu na kuchukuwa mkopo pasipo muhusika kujua jambo linalopelekea nyumba na Mali za watu kupigwa mnada na kuacha familia zikikosa makazi.
Aidha RC Makonda amewataka madalali wa mahakama na wale wa mabenki kuhakikisha wanatoa taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa mtaa kabla ya kufanya mnada huku akiwaagiza kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa ndani ya chama cha madalali ili kuondokana na uvunjifu wa amani wakati wa minada.
Pamoja na hayo RC Makonda amewataka wenyeviti wa mitaa kusimamia sheria na taratibu kwa kuhakikisha minada inafanyika posipo uonevu wala uvunjifu wa amani.
RC Makonda pia amewaagiza watu wa Benki kuhakikisha Maafisa Mikopo na Wanasheria wao wanazingatia taratibu baada ya kubaini baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro na utapeli.
Mbali na hayo RC Makonda amewapa mwezi mmoja watu wa Mabenki, Wenyeviti wa Mitaa, Madalali wa Mahakama na Mabenki kuandika changamoto na mapendekezo yao kisha kuyawasilisha kwake kwaajili ya kufanyiwa marekebisho na mwisho wa siku tuwe na sheria nzuri inayomlinda mkopeshaji na mkopwaji.
Hata hivyo RC Makonda amewataka wote wanaokopesha wananchi mitaani kienyeji pasipo kusajiliwa wala kuwa na vibali vya utambuzi kuacha Mara moja kwakuwa wamekuwa chanzo cha migogoro huku akiwataka madalali wa nyumba,viwanja na mashamba kuhakikisha wanasajiliwa na kutambulika na serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa