Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametoa miezi minne kwa waajiri wa Makampuni na Mashirika kuhakikisha wanawaajiri watu wenye ulemavu Kama Sheria ya Walemavu ya 2010 na Mikataba ya kimataifa ya mwaka 2006 iliyoridhiwa na Tanzania mwaka 2009 sura ya 27 inavyowaaagiza kufanya hivyo.
RC Makonda amesema ifikapo Mwezi January mwakani ataanza ziara ya kutembelea kwenye kila Kampuni na Taasisi Jijini humo kukagua Kama wametekeleza Sheria na agizo hilo ambapo watakaobainika kukaidi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha RC Makonda amesema kitendo cha kuwaajiri walemavu kitapunguza ongezeko la ombaomba, ukatili, utupwaji wa watoto wenye ulemavu, kuhamasisha walemavu kusoma pamoja na kuwawezesha walemavu kuhudumia familia zao.
"Hatuwezi kuwa na ndugu zetu wamesoma na wanasifa za kupata Kazi lakini tunawanyima matokeo yake wengine wanaishia kujinyonga, kinamama wanatupa Watoto wenye ulemavu, mila potovu zinaendelea kupoteza haki na mwisho wanabaki wakiwa Masikini na kushindwa hata kumudu gharama za Matibabu, Jambo hili sio la kufumbia macho" alisema RC Makonda
Kwa mujibu wa Sheria ya ajira kwa watu wenye ulemavu No. 9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31 inamtaka kila mwajiri mwenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha 3% ya wafanyakazi ni watu wenye ulemavu.
RAIS MAGUFULI AMEONYESHA DIRA KWA KUTOA KIPAUMBELE CHA AJIRA KWA WALEMAVU, NI WAKATI SASA KWA WAAJIRI KUTEKELEZA SHERIA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa