Kilio cha muda mrefu cha walimu wa shule ya msingi Vijibweni Wilaya ya Kigamboni kufanya kazi chini ya Miti, kwenye makorido, kwenye madawati na kujisaidia kwa majirani kutokana na ukosefu wa ofisi ya walimu leo kimepatiwa ufumbuzi baada ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda kuwapatia ofisi ya kisasa yenye hadhi ya kimataifa.
Ofisi hiyo ya kisasa aliyokabidhi RC Makonda ujenzi wake umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 200 ambapo ndani yake ina ukumbi mikutano, Ofisi ya mwalimu mkuu, Mwalimu mkuu msaidizi,ofisi ya walimu wote, Chumba cha kuhifadhi mitihani, stoo, sehemu ya mapokezi, chumba cha kubadilishia nguo, vyoo vya kisasa na bafu huku ikiwa imefungwa viyoyozi (AC) ili kuhakikisha walimu wanafanya kazi kwa uhuru.
Akizindua ofisi hizo RC Makonda amesema dhamira yake ya kuhakikisha walimu wanafanya kazi katika mazingira bora ipo palepale kwakuwa anatambua thamani ya mwalimu ni kubwa kwenye jamii hivyo wanastahili kupewa heshima.
Aidha RC Makonda ameishukuru Kampuni ya CRJE East Afrika ya Nchini China iliyoamua kumuunga mkono kwa kujenga ofisi mbili za walimu kwa lengo la kuwawezesha walimu kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Kwa upande wao walimu wa Shule ya Vijibweni kwanza wamemshukuru RC Makonda kwa kuwajengea Ofisi hiyo ya kisasa kwakuwa awali walikuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo chini ya miti na wamekuwa wakitumia choo kimoja na wanafunzi na wakati mwingine kujisaidia kwa majirani wema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa