Mkoa wa Dar es salaam umetekeleza maelekezo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuanzisha Bima ya Afya ya Wananchi ambayo inawawezesha wafanyakazi walio kwenye Sekta isiyo rasmi kupata huduma za matibabu ya uhakika mwaka mzima kwa gharama sawa na Bure.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amesema Bima hiyo itawawezesha wananchi wakiwemo wamachinga, bodaboda, mama Lishe, Baamedi, wavuzi, wakaanga chipsi, Vinyozi na wengineo kupata matibabu kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa familia ya watu 6 ambayo ni sawa na Shilingi 25,000 kwa kila kichwa huku kwa mtu asie na familia akihitajika kutoa 40,000 pekee kwa mwaka mzima.
RC Makonda amesema wananchi wengi wamejikuta wakiingia kwenye umasikini kwa kuuza Mali walizozitafuta kwa tabu ikiwemo Viwanja, Nyumba, mashamba, gari, pikipiki au kupitisha michango ili waweze kugharamia matibabu lakini kupitia bima hii itawezesha familia kupata matibabu kwa gharama nafuu kabisa kwenye hospital na kituo chochote cha Afya cha serikali mkoani humo.
"Tumeshuhudia watu wengi wakijikuta maskini baada ya kuugua, unakuta familia anaumwa baba, mama na watoto sasa ukipigia mahesabu gharama za matibabu wanatumia zaidi ya laki tano kwa wakati mmoja, lakini wangekuwa na Kadi ya Bima wangepata matibabu na kuokoa gharama zote hizo, niwasii Sana sana wananchi wajikatie Bima hii ya Wananchi,huu Ndio ukombozi " Alisema RC Makonda.
Pamoja na hayo RC Makonda amewahimiza viongozi wa Dini na mitandao ya kijamii kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya ya Wananchi.
DAR ES SALAAM HATUTAKI KUONA UGONJWA UNAMFANYA MTU KUWA MASKINI, TUMIA BIMA YA AFYA YA WANANCHI KWA UHAKIKA WA MATIBABU.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa