Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuweka mkazo na kusimamia ipasavyo suala la lishe katika maeneo yao na kufanya Mkoa huo kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na wakazi wenye afya bora.
RC Makonda amesema hayo leo wakati wa kikao cha utilianaji saini wa mkataba wa lishe baina yake na Wakuu wa Wilaya ambapo amesema suala la lishe duni limekuwa tatizo kubwa linalopelekea matatizo ya uwezo mdogo wa kufikiri, udumavu, utapia mlo, idadi ya watoto njiti, watoto wanaozaliwa na mgongo wazi, vichwa vikubwa, uono hafifu, ukosefu wa damu, vitamin na tatizo la ukondefu.
Aidha RC Makonda amesema Mkoa umejidhatiti kukabiliana na tatizo la lishe kwa kutoa elimu ya lishe, kuzuia magonjwa ya upungufu wa viini lishe, kuongeza virutubisho kwenye chakula pamoja na matibabu ya utapiamlo.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema takwimu za lishe Mkoa wa Dar es salaam Mwaka 2015 zinaonyesha 14.6% sawa na watoto 91,104 kati ya watoto 624,000 wana Utapiamlo (udumavu) sugu, 4.7% sawa na watoto 23,000 Kati ya watoto 624,000 wana Ukondefu, 59.4% sawa na watoto 371,280 Kati ya watoto 624,000 wenye umri chini ya miaka 5 wana upungufu wa damu na 53.3% sawa na kinamama 332,592 Kati ya 624,000 walio kwenye umri wa kuzaa wana upungufu wa damu hali inayoonyesha kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kukabiliana na tatizo la lishe duni.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Afya athari za kudumu za ukosefu wa Lishe hutokea siku 1,000 za kwanza kuanzia wakati wa ujauzito hadi pale mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa