Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewaagiza wakuu wa Wilaya kuhakikisha hadi kufikia 01/03/2019 kila mfanyabiashara mdogomdogo anakuwa na Kitambulisho cha utambuzi kilichotolewa Na Rais Dkt. John Pombe Magufuli huku akiwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo.
RC Makonda amesema kuwa baada ya Tar 01/03/2019 mfanyabiashara yoyote atakaekutwa hana kitambulisho, leseni ya manispaa au vielelezo vya kukipa kodi TRA atajikuta mikononi mwa vyombo vya dola kama muhujumu Uchumi.
Mhe. Makonda ameyaeleza hayo leo wakati wa kikao na watendaji wote wa mkoa kilichoenda sambamba na kugawa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogowadogo kwa Wakuu wa Wilaya na kufanya mkoa huo kuwa kinara kwa kupokea takribani vitambulisho 175,0000 kutoka kwa Rais Magufuli.
Aidha RC Makonda amesema baada ya 01/03/2019 serikali ya mkoa itawaingiza wafanyabiashara hao katika mfumo wa kisasa (Database) utakaowezesha serikali kuwafikia na kuwapa mafunzo ya namna kukuza biashara zao ili mwisho wa siku wafikie uchumi wa Kati.
Pamoja na hayo RC Makonda amewatahadharisha watendaji wanaowatoza kiasi kikubwa cha fedha ya kitambulisho tofauti na bei elekezi ya Tsh 20,000 huku akiwahimiza wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo waliyopewa na Rais.
Mbali na Vitambulisho RC Makonda ametoa miezi miwili kwa Wakurugenzi wa Manispaa kuhakikisha Leseni za wafanyabiashara zinaingizwa katika mfumo mmoja ikiwa ni pamoja na kuharakisha utoaji wa leseni ili kupunguza usumbufu kwa wananchi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa