Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amegoma kukabidhi kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Manispaa ya Ubungo kutokana na ujenzi huo kusuasua hadi sasa ambapo amemtaka Mkandarasi wa ujenzi huo Wakala wa Ujenzi TBA kuhakikisha anakabidhi mradi ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo.
RC Makonda amechukizwa kuona ujenzi huo ulitakiwa kukamilika na kukabidhiwa Mwezi Disemba mwaka jana lakini mkandarasi aliomba kuongezewa miezi sita lakini hadi sasa ujenzi haujakamilika jambo lonaloendelea kuwafanya Watumishi wa Manispaa hiyo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Hayo yamejiri wakati wa mwendelezo wa ziara ya RC Makonda kukabidhi miradi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo kwa siku ya leo amekabidhi miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 196.4 kwa upande wa Jimbo la Kibamba.
Miongoni mwa miradi aliyokabidhi RC Makonda ni Standi ya Mabasi ya Mikoani ya Mbezi Luis inayogharimu Bilioni 50, Upanuzi wa Barabara ya Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa Km 19.2 na gharama ya Bilioni 140.4, Upanuzi wa Mtambo wa Maji Ruvu Juu na ujenzi wa Tank Kibamba wa thamani ya Milioni 624.
Aidha RC Makonda pia amekabidhi mradi wa ujenzi wa mabanda saba ya wafanyabiashara Mbezi Luis unaogharimu Bilioni 1.5 na ujenzi wa Kituo cha Afya Kimara Bilioni 1.5.
Ziara ya RC Makonda itaendelea siku ya kesho kwenye Jimbo la Ubungo ambapo atakabidhi miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa