Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametegua kitendawili kilichowatesa kwa muda mrefu wakazi wa Kata ya Liwiti baada ya mmoja wa wananchi kudai ndie mmilika halali wa eneo la Soko lao jambo lililotaka kupelekea uvunjifu wa Amani.
Akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara na wananchi hao RC Makonda ameagiza eneo hilo kurejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya matumizi ya Soko baada ya kubainika kuwa anaedai eneo hilo aliuziwa kihalali alijichanganya badala ya kwenda kiwanja kilichopo Block No. 200A kujikuta anakwenda Block No. 200B ambacho kwa mujibu wa Ramani ya Mipango miji ni eneo la Umma.
Kutokana na Mkanganyiko huo RC Makonda ameagiza Mama huyo kuonyeshwa kiwanja chake Block No. 200A na kuagiza asitokee mtu yoyote wa kuwabugudhi wananchi na eneo lao la soko.
Aidha RC Makonda ameagiza kuvunjwa Mara moja kwa ukuta mmoja wa mwananchi aliyejenga kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa mtaa wa Amani Kata ya Tabata Liwiti kukosa sehemu ya kupita na kujikuta wanazunguka umbali mrefu.
Pamoja na hayo RC Makonda pia ameagiza Uwanja wa mpira wa Tabata Sigara kurejeshwa kwa wananchi kwaajili ya matumizi ya michezo baada ya wananchi kulalamika kuwa aliyenunua Magorofa ya Sigara anadai kuwa amenunua pia eneo la Kiwanja na kusababisha kukosekana kwa eneo la michezo.
Sambamba na hayo RC Makonda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Segerea Mhe. Bona Kalua kwa kuendelea kuwasemea wananchi juu ya kero zinazowasumbua hadi kuzifikisha ofisi ya Mkuu wa mkoa.
Kwa upande wao wakazi wa Kata ya Liwiti wamefurahia kuona migogoro yao ya muda mrefu imetatuliwa kwa mpigo ambapo wamempongeza RC Makonda kwa usimamizi mzuri wa sheria huku wakimpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwateulia Mkuu wa Mkoa anaewafuata na kuwasikiliza wananchi wake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa