Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda leo amepokea wageni 18 kutoka Nchini Marekani ambao ni walimu wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo waliokuja Nchini kujifunza Utamaduni wa Tanzania.
Ugeni huu ni kutokana na mahusiano aliyoyajenga kipindi akiwa nchini Marekani wakati wa likizo yake mwishoni mwa mwaka jana.
Katika mazungumzo ya pamoja na Mkuu wa Mkoa Mh. Paul Makonda amewasilisha kwa walimu hao kutoka majimbo mbalimbali nchini Marekani maombi mawili, ambayo ni Ujenzi wa Maktaba ya kisasa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam, kwani hitaji la kusoma kwa wananchi wa kawaida ni kubwa na kutokana na uhaba wa maktaba rafiki kwa kada zote hapa jijini.
Maktaba hii pia itasaidia upanuzi wa uelewa wa mambo mbalimbali katika nyanja za uchumi, siasa, kilimo, tehama na teknolojia za kisasa katika sekta za madini, misitu ya asili, mito, maziwa na wanyama adimu wanaopatikana nchini Tanzania tu.
Lengo ni kumuwezesha mkazi wa Dar es salaam kuwa na uelewa mpana wa mambo na kujadiri mambo ya kitaifa na kidunia kwa utafiti mkubwa zaidi.
Na pia uanzishwaji wa programu maalum ya kuleta walimu wa ngazi mbalimbali kutoka nchini Marekani kwa ajili ya kufundisha shule za Mkoa wa Dar es salaam. Hitaji la walimu hawa ni jibu la changamoto kubwa ya ukosefu wa walimu wa sayansi na Tehama nchini.
Maombi hayo mawili yamepokelewa na kikundi hicho cha walimu na kuongeza kuwa wapo tayari kuanza ujenzi wa maktaba hiyo endapo ofisi ya Mkoa itatoa eneo la ujenzi wa Maktaba hiyo, lakini pia watatoa jumla ya nakala 59,000 ya vitabu mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya maktaba hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mh. Makonda alisema, “Mimi ningependa Wanafunzi wa Mkoa wa Dar es salaam wajue Dunia inaendaje, na mkakati tulionao na ndugu zangu hawa 18 ambao wengine ni Mabosi wakubwa Marekani ni kuwa na umoja wa kuwa na utaratibu wa kuletewa walimu kutoka nchini humo, hii itatusaidia sana”.
Kwa upande wake kiongozi wa msafara huo Dr. Fredoline Anunobi amesema kuwa watahakikisha wanajenga Maktaba hiyo ya kijamii kwa wakati ili kuwezesha wananchi kupata huduma muhimu ya elimu muhimu na pamoja na kuwaleta walimu wa masomo ya sayansi na tehama katika mkoa wa Dar es salaam.
Mratibu wa Mipango kutoka Albany Community Charter School Shannari Akosua kutoka Marekani alimshukuru Mkuu wa Mkoa kuwakaribisha vizuri na kueleza kuwa wamefurahi kuwepo katika mkoa wa Dar es salaam na kwa namna ya kipekee ambavyo Mkoa unajenga mahusiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na kuahidi kushawishi taasisi nyingi zaidi kutoka nchini Marekani kufanya kazi na Mh. Makonda katika kuendeleza mkoa wa Dar es salaam.
Bi. Shannari alisisitiza kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya utalii viliopo nchini sambamba na lugha adhimu ya kiswahili ambayo ni moja ya mambo waliyojifunza kutoka hapa nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa