Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amefanya ziara kwenye Jimbo la Kawe kwa lengo la kukabidhi Miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano kwa Chama cha Mapinduzi CCM ikiwa ni utekelezaji wa ahadi alizozitoa Rais Dkt. John Magufuli kupitia ilani ya Chama hicho.
Miongoni mwa miradi aliyokabidhi RC Makonda ni Mradi Mkubwa kabisa wa Kuchakata taka wenye thamani ya Bilioni 5.59 uliopo Mwabwepande, Mradi wa Shule Mpya ya sekondari ya Mabwe Tumaini Girls iliyogharimu Shilingi Bilioni 2.6 na Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Kinondoni iliyopo Mabwepande yenye thamani ya Bilioni 2.4.
Aidha RC Makonda amekabidhi pia Mradi wa Matanki makubwa matano na Pampu za kusambaza Maji zilizopo Changanyikeni, Ujenzi wa Kituo cha Afya Bunju chenye thamani ya milioni 600, Mradi wa Makazi ya Askari Mabwepande pamoja na kukabidhi Zahanati ya Mkoroshini kata ya Msasani yenye thamani ya Milioni 408.
Akizungumza katika ziara hiyo RC Makonda amewahimiza wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi watakaowaletea maendeleo na sio viongozi wanaopinga kila jambo jema linalofanywa na serikali.
Hata hivyo RC Makonda amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Kawe ili kusogeza huduma za Afya kwa wananchi wa kata hiyo.
Kesho RC Makonda ataendelea na ziara yake ya kukabidhi miradi kwa Chama cha Mapinduzi CCM kwa upande wa Jimbo la Kinondoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa