- Aagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kusimamia usafi ndani ya wiki moja kuanzia leo
- Awataka Watendaji wa Kata na Mitaa kuyalinda maeneo yasiwekwe vibanda tena
- Asema kila Taasisi ya Umma kulinda eneo lake
- Asisitiza kufikia Oktoba 30, 2021 hataki kuona kibanda chochote kwenye "Road Reserve"
- Ameendelea kupongeza uongozi wa Machinga DSM kwa kushirikiana na Serikali
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makalla leo Oktoba 20, 2021 amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika Mkoa wa DSM kuhakikisha maeneo yote ambayo Machinga wanahama yanafanyiwa usafi ndani ya Wiki moja kuanzia leo.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo wakati anaongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano Arnatoglo-Ilala Jijini Dar es Salaam.
Mhe Makalla amewataka Watendaji wa Kata na Mitaa kuyalinda maeneo katika Kata au mitaa yao, kwa kuwa wamachinga sasa wanahama kwenda maeneo sahihi waliyowapanga hatarajii kuona wafanyabiashara hao wanarudi tena katika maeneo ya awali wakati Mtendaji wa Kata au Mtaa husika yupo.
Mhe Mkuu wa Mkoa pia amezitaka Taasisi zote za Umma ambazo ziko katika Mkoa wa Dar es Salaam kulinda maeneo yake yasivamiwe tena na wafanyabiashara wadogo.
Mhe Makalla amesema ifikapo Oktoba 30, 2021 hataki kuona kibanda chochote kwenye "Road Reserve" ametolea mfano barabara ya Morogoro na Barabara ya Airport.
Aidha Mhe Makalla amebainisha ndani siku 12 alizoongeza ni matarajio yake *Mitaro na mifereji itakuwa wazi, Njia za watembea kwa miguu zitakuwa wazi na safi, hakutakuwa na wafanyabiashara walio mbele ya maduka ya wengine, Mitaa iwe safi na inapitika*
Sambamba na hilo Mhe Makalla amesema anamshukuru Mungu zoezi la kuwapanga wamachinga Vizuri linaendelea vema tena kwa mafanikio makubwa, amewashukuru wamachinga na kuupongeza uongozi wa wamachinga DSM kwa kujitambua na kushirikiana vizuri na Serikali ni imani yake kuwa DSM sasa inaenda kuwa safi na inayovutia.
Mkuu wa Mkoa amesema ukiangalia sababu kubwa inayofanya Dar es Salaam kuwa chafu ni biashara holela hivyo zoezi la kuwapanga vizuri wamachinga likikamilika atazindua rasmi kampeni ya usafi DSM
Dar es salaam safi na inayovutia inawezekana tuendelee kutoa Elimu kila mmachinga afanye biashara katika sehemu sahihi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa