-Amuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kuendelea kutoa huduma kesho Agosti 23, 2021 katika uwanja wa Uhuru
-Awaagiza wakuu wa Wilaya katika maeneo yao kuendeleza utaratibu wa kutenga maeneo ya wazi kuwapatia chanjo wananchi
-Asisitiza amekuwa akiendelea kupokea maombi mengi kutoka makundi anuai kama Bodaboda, Bajaji, madereva wa magari makubwa na wengine wengi
Mhe Amos Makalla akishuhudia mmoja kati ya maelfu walijitokeza kupata chanjo ya UVIKO - 19 uwanja wa Uhuru mapema leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Amos Makalla ametembelea viwanja vya Uhuru Temeke kujionea mwenendo wa utoaji chanjo ya UVIKO-19 kufuatia tamko lake kwa umma la kutoa huduma hiyo kwa uwazi siku ya Jumapili Agosti 22, 2021 ambayo ni leo.
Mhe Makalla akipita kukagua namna zoezi la chanjo ya UVIKO-19 linavyoendelea katika Uwanja wa Uhuru.
Akiwa katika uwanja wa Uhuru Mhe Makalla amejionea muitikio mkubwa na kumlazimu kumuagiza Mganga Mkuu Mkoa Dkt Rashid Mfaume kuendelea na huduma hiyo uwanjani hapo kesho.
Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa amesema nimekuwa nikiendelea kupokea maombi mengi kutoka makundi mbalimbali na hiyo inatokana na zoezi hilo kuendeshwa kwa kuangalia makundi maalum hususani watu wenye zaidi ya miaka 50 na wale walioko katika mazingira hatarishi.
Hivyo wale wa miaka 18 na kuendelea kuikosa fursa hiyo ndio maana Mkoa ukaona kuna kila sababu ya kutenga siku na sehemu ya wazi ili wananchi wapate huduma hiyo kwa urahisi.
"Zoezi hili limefanikiwa kama mnavyo ona, niwashukuru wananchi wanaoendelea kupata chanjo nitoe rai msiwe na wasiwasi hata mimi Mkuu wenu wa Mkoa na Katibu Tawala hapa nimeshachanja na niko vizurii.. safiii kabisa" Alisema Mhe Makalla
Aidha amewaagiza wakuu wa Wilaya katika maeneo yao kuendelea na huduma hiyo kwa kutenga maeneo ya wazi ili wale wote wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea wapate chanjo.
Vilevile Mhe Makalla amesema katika uwanja huo wa Uhuru watu 100 hupata huduma ya chanjo kwa wakati mmoja na kwa taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa Mkoa takwimu za waliochanja ukiunganisha na wa siku ya leo hadi kufikia saa 4 asubuhi ni zaidi ya watu 2882
Chanjo hii ni bora, Salama, na yenye Ufanisi Mzuri
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa