Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge leo tarehe 17 Septemba, 2020 amefanya ziara ya kukagua miradi iliyopo katika Wilaya za Kinondoni, Ubungo, na Ilala na kutaka miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Awali Mhe. Kunenge alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tegeta Nyuki yenye urefu wa kilometa 1.06 inayosimamiwa na Tarura na kujengwa na kampuni ya CMG Construction iliyopo katika Wilaya ya Kinondoni ambapo alimtaka mkandarasi wa mradi huo kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwani amekua akisuasua kumaliza mradi huo licha ya kuongezewa muda.
“Wakandarasi wasipofanya kwa wakati waliopewa wanaongeza kero kwa wananchi, hivyo naagiza mradi huu uwe umekamilika kwa kiwango cha rami na mitaro mizuri ilfikapo Oktoba mwishoni”. Aliagiza RC Kunenge
Baada ya hapo msafara wa Mhe. Mkuu wa Mkoa ulielekea katika ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Madale kuelekea Wazo yenye urefu wa Kilomita 6 inayogharimu kiasi cha Tshilingi Billioni 9.9 ambapo Mkuu huyo wa Mkoa alifurahishwa na juhudi za usimamizi na ujenzi wa mradi huo ambapo alisema mkandarasi wa mradi huo yupo ndani ya muda na ujenzi huo unaenda vizuri. Alimtaka mkandarasi huyo pia asibweteke bali aukamilishe mradi huo ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, RC Kunenge pia ametembelea na kukagua Mradi wa ujenzi wa Stand Mpya ya mabasi ya kisasa ya Mbezi Louis ambayo ujenzi wake umefika 80% na inagharimu Kiasi cha Shilingi Bilioni 56 ambapo ameonyesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia.
Mwisho kabisa RC Kunenge ametembelea ujenzi wa Daraja la Ulongoni A lililopo Kata ya Gongolamboto ambalo ujenzi wake unagharimu Shilingi Bilioni 4.3 na unatarajia kukamilika ifikapo Aprili, 2021 na Ujenzi wa Daraja la Ulongoni B ambapo amewahimiza wakandarasi kuongeza juhudi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi ukamilike ndani ya Muda uliopangwa ili kupunguza kero walizokuwa wakizipata wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Ulongoni A Bw. Ibrahimu Hamisi alitoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali na kuwatengea kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwani changamoto katika madaraja hayo ni kubwa hasa katika upitaji wa watu, magari, pikipiki na bajaji.
“Mchakato unavyoendelea tunaamini inaweza ikawa faraja kwetu” Alisema Mwenyekiti wa Ulongoni A Bw. Ibrahimu Hamisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa