Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila Leo Novemba 9,2024 amezindua mpango maalum wa upandaji wa miti kandokando ya Mto Mpiji katika eneo la Mabwepande.
Mpango huu unahusisha upandaji wa miche ya michikichi zaidi ya 5,000 kwa lengo la kulinda kingo za mto na kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mvua zinaponyesha kwa wingi. Mradi huu unalenga kuongeza uoto wa asili na kusaidia kudhibiti mtiririko wa maji yanayovunja kingo za mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Aidha ilielezwa kuwa moja ya changamoto kubwa katika eneo hili ni maji kujaa mchanga mtoni na hivyo kusababisha mto kutanuka na kuleta madhara makubwa kwa jamii inayozunguka. Kupitia mpango huu wa upandaji miti, inatarajiwa kuwa tatizo hili litapungua na mazingira yatakuwa rafiki zaidi kwa maendeleo endelevu ya eneo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Tawala wa Manispaa ya Kinondoni Warda Obathany alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali katika kufanikisha mpango huu utakaosaidia katika kulinda kingo za mito, bali pia utachangia katika kuboresha hali ya hewa kwa kuingiza hewa safi kutokana na miti hiyo.
Wadau mbalimbali waliokuja kushiriki hafla hiyo walionesha matumaini yao na kupongeza juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira na kusema kupitia mpango huu, wananchi wataelimika zaidi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi ya aina hii.
Huu ni mwanzo mzuri kwa jiji la Dar es Salaam katika kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira,RC Chalamila amehitimisha kwa kusema Serikali imejipanga kuhakikisha mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na kuahidi kuendelea kuleta miradi zaidi ya mazingira kwa manufaa ya wananchi na mazingira ya Mkoa huo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa