-Aishukuru kampuni ya Lake Gas kwa kutoa mitungi 1000 kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais ya Nishati safi.
-Atangaza Tamasha kubwa la Mapishi Septemba 23/2024 kwa kutumia nishati safi.
-Asema tumezindua kampeni ya matumizi ya Nishati safi katika Mkoa, kampeni hii itakua endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila Leo Septemba 12,2024 amezindua kongamano la matumizi ya Nishati safi ya kupikia katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambalo limehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Mameya, Wakurugenzi wa Halmashauri,Watendaji Wakuu wa Taasisi ambata za Nishati safi, Viongozi wa dini na mamia ya mama lishe na baba lishe. Akizindua kongamano hilo RC Chalamila ameishukuru kampuni ya Lake Gas kwa kutoa mitungi 1000 ya Nishati safi ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuachana na matumizi ya Nishati chafu badala yake kutumia Nishati safi ya kupikia. "Niwaombe Taasisi, Mashirika na wadau wengine ndani ya Mkoa kuiga mfano wa kampuni ya Lake Gas kuendelea kutoa mitungi zaidi ya gesi ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi." Alisema RC Chalamila.
RC Chalamila kupitia kongamano hilo ametangaza Tamasha kubwa la Mapishi kwa kutumia Nishati safi ndani ya Mkoa huo Septemba 23,2024 ambalo litaambatana na Mapishi ya aina mbalimbali kama vile nyama choma,mbuzi choma,samaki choma na pilau vilevile amehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi na kuahidi kutoa ofa maalum kwa watu 1000 watakaowahi kufika kwenye Tamasha hilo. Eneo la kufanyika kwa Tamasha hilo litatangazwa siku za usoni.
Aidha Mhe.Chalamila amesema leo tumezindua kongamano la matumizi ya Nishati safi ya kupikia katika Mkoa wetu, kampeni hii ni endelevu tukiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya "Jali Afya, Pika Kijanja, Tumia Nishati Safi Okoa Mazingira Kwa Ukuaji wa Uchumi".
Sanjari na hilo RC Chalamila amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuratibu upatikanaji wa mitungi ya gesi kutoka Taasisi mbalimbali za serikali kuchangia mitungi kuanzia 200 hadi 300 kabla ya Septemba 30/2024.
Kwa upande wa muwakilishi wa Mtendaji Mkuu kampuni ya Lake Gas Bw. Stephen Mtemi amesema kampuni ya Lake gas itaendelea kushirikiana na mkoa wa Dar es Salaam kuwafikia wananchi wengi zaidi pia ameishukuru Wizara ya Nishati na wakala wa Nishati vijijini kwa kuwapatia nafasi ya kusambaza majiko ya gesi kwa watanzania wenzetu wa mijini na vijijini hivyo amewaasa watanzania kuendelea kuunga mkono juhudu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutumia Nishati safi.
Mwisho RC Chalamila amewahakikishia watanzania hususani wakazi wa Mkoa huo kuwa hali ya usalama ni shwari, wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato pasipo na shaka yoyote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa