-Asema upatikanaji wa fedha hizo utawezesha upanuzi na ukarabati wa majengo ya Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa
-Atoa rai kwa wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchangia
-Abainisha kilele cha Harambee hiyo ni Agosti 31,2024 katika ukumbi wa Mlimani City
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albaert Chalamila leo Julai 05,2024 amezindua harambee kabambe ya kuchangia upanuzi na ukarabati wa majengo ya hospitali ya Rufaa ya Amana, ambapo harambee hiyo inalenga kukusanya zaidi ya bilioni 3.
Akiongea katika hafla hiyo iliyofanyika katika viunga vya Hospital ya Amana RC Chalamila amemshukukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya na anaendelea kufanya katika sekta ya Afya hapa nchini hususani Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo kupitia juhudi hizo ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa sekta ya Afya kuunga mkono juhudi za Mhe Rais kwa masilahi mapana ya ustawi wa jamii.
Aidha RC Chalamila amesema kwa sasa itafanyika harambee yenye lengo la kukusanya zaidi ya bilioni tatu kuwezesha ukarabati na upanuzi wa majengo ambayo yapo na yatabeba huduma nyingine wakati tutakapoanza kubomoa baadhi ya majengo yatakayo bomolewa kupisha mradi huo mkubwa na wa kihistoria ikiwa ni kuendeleza kuunga mkono juhudi za Mhe Rais “Leo Julai 05,2024 ni uzinduzi rasmi na kilele chake ni Agosti 31,2024 katika ukumbi wa mlimani City mgeni rasmi anatarajiwa kuwa kiongozi wa kitaifa ambapo taarifa rasmi itatolewa hivyo tuendelee kujipanga vizuri kwa ajili ya siku hiyo” Alisema RC Chalamila.
Kwa Upande wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt Kiwelu amesema unaweza kuona kwa sasa majengo yako mithili ya kijiji cha ujamaa na mpango mpya yako machache na yaliyopangwa kwa hekima. Hivyo kupitia harambee hiyo jengo jipya la huduma za mama na mtoto ambalo litajengwa Amana litakuwa lenye vitanda zaidi ya 350 pia jengo la Utawala la kisasa ambapo utofauti katika jengo la utawala ni kuwa kutakuwa na makumbusho (Museum) ambayo itakusanya historia nzima ya Afya nchini Tanzania.
Vilevile Jengo hilo litakuwa na maabara za kisasa za kujifunzia kwa vitendo (clinical skills laboratories), madarasa, kumbi za mikutano, ofisi, kutakuwa na huduma za kibenki, maduka ya vifaa tiba, supermarket, hoteli na zaidi kutakuwa na ukuta wa dhahabu ambapo majina ya wote watakaochangia hospitali hii yatatunzwa kama kumbukumbu ya vizazi vijavyo kudhihirisha nguvu ya umoja wetu. “Hatutaki maisha ya kuishi kwa nadharia tunataka kuwarahisishia maisha watoto wetu kujua historia ya sekta ya Afya ndani ya muda mfupi wafikapo Amana” Alisema Dkt Kiwelu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa