-Apokea matembezi ya wanafunzi katika shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani
-Ataka Jamii kujivunia Lugha ya Kiswahili
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Julai 05,2024 ameungana na mamia ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani maadhimisho ambayo yamefanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama Wilaya ya Kinondoni.
RC Chalamila akiwa mgeni rasmi wa tukio hilo amepokea matembezi ya wanafunzi yaliyoongozwa na Brass Bend ya Jeshi la Magereza na baadaye alipata wasaa wa kutoa hotuba.
RC Chalamila akiongea na mamia ya wanafunzi katika maadhimisho hayo amesema ni muhimu kueneza utambuzi wa lugha ya Kiswahili katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni ambapo alisema kwa sasa Kiswahili kinafanya vizuri hapa nchini na kwingineko Duniani ni vema kuendelea kueneza utambuzi zaidi wa lugha hiyo
Aidha ameitaka jamii kujivunia lugha ya Kiswahili ambapo amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Kiswahili kinakua ndani na nje ya nchi hivyo ametoa pongezi kwa wale wote wanaopigania makuzi ya Lugha hiyo hususani wanafunzi vilevile ametoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mashindano ya uandishi wa Insha kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Saad Mtambule amesema lugha ya Kiswahili sio tu inatuunganisha bali ni kielelezo cha utamaduni wetu hivyo ni lazima tutumie Kiswahili na tuzungumze lugha hiyo kwa kujidai kabisa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa