Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila Leo Oktoba 11,2024 amegawa mitungi ya gesi kutoka 'PUMA ENERGY' iliyofanyika katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni, tukio ambalo lilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya,Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi pamoja na makundi mbalimbali ya kina mama lishe na baba lishe.
Kufanyika kwa tukio hilo ni mwendelezo wa kuunga mkono kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa kutumia Nishati Safi ambapo zaidi ya mitungi 800 ya gesi imetolewa kwa makundi mbalimbali ili waweze kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi endelevu ya Nishati safi.
Aidha Mhe. Chalamila ameeleza umuhimu wa matumizi ya Nishati safi kama njia ya kuokoa kizazi cha kina mama kuondokana na matumizi ya Nishati chafu ambayo hudhoofisha Afya ya kina mama kupitia magonjwa mbalimbali kama vile ugonjwa wa mapafu,hivyo kwa kutumia Nishati safi itaweza kumsaidia mama kuepukana na athari hizo.
Vilevile RC Chalamila ametangaza kuwepo kwa Tamasha la Mapishi kwa kutumia Nishati safi siku ya Jumamosi, Novemba 2,2024 katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni na kutoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Halima Bulembo akisaidiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutafuta fedha isiyopungua Mil.100 kwa ajili ya watu 2000 watakaowahi kufika katika Tamasha hilo.
Pia RC Chalamila amewaagiza Wakuu wa Wilaya ya Temeke,Ilala,Kinondoni na Ubungo kushirikiana kuratibu siku ya Tamasha la Mapishi ambalo litaambatana na 'Jogging club' watakaoanzia Magomeni mpka Biafra, kuandaa Ng'ombe watakaochinjwa na kuliwa siku hiyo, pamoja na kukaribisha makampuni ya vinywaji kama TBL,SBL,KONYAGI, PEPSI na COCA COLA kuja kuunga mkono na kujumuika katika Tamasha hilo.
Mwisho, Mkurugenzi Mtendaji wa PUMA GAS Bi.Fatma Abdallah ameelezea matokeo ya kutumia Nishati safi kama njia rahisi na salama ya kupikia na kulinda Afya ya Mama na makazi yake kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa