Ndugu Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha juu ya ujio wa Ugeni wa Rais wa Uganda Mhe.Yoweri Kaguta Museveni.
Rais Museven anatarajiwa kufika nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja siku ya alhamisi ya tarehe 09/08/2018 Majira ya Aubuhi na kupokelewa na Mwenyeji wake hapa nchini, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere (Terminal One) na kuelekea Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya kikazi na baadae saa nane mchana ataondoka hapa nchini.
Ugeni huu ni maalum kabisa katika kudumisha mahusiano ya Nchi hizi mbili ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu Nchi ya Uganda na Tanzania zimekuwa katika mahusiano ya Kiuchumi hasa katika sekta ya Usafirishaji ambayo tumeshuhudia kufufuliwa kwa safari za kusafirisha mizigo kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kwenda Uganda, pamoja na hayo nchi ya Uganda (ambayo ni landrocked ) ni mtumiaji Mkubwa wa Bandari zetu za Tanga na Dar es salaam katika kupitisha mizigo yake kutoka nchi za nje, lakini pia si haya tu, tunashuhudia kwa sasa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Tanga kwenda Hoima Nchini Uganda unaodhihirisha wazi kuwa nchi ya Uganda na Tanzania ni marafiki wanaotegemeana kwenye mambo mengi.
Ujio wa Mh Rais Museveni unazidi kudhihirisha kuwa Serikali yetu ya awamu ya tano chini ya uongozi uliotukuka wa Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli inaheshimika na kuthaminiwa katika siasa za kimataifa.
Kwa kutambua ugeni huu sisi kama wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania tunamkaribisha mgeni wetu na ajisikie kuwa yuko nyumbani muda wote atakapokuwa hapa jijini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa