Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul C. Makonda akiambatana na viongozi waandamizi wa Mkoa na Mamlaka ya Maji safi na Maji taka DAWASA wametembelea miradi mikubwa ya uchimbaji wa visima vikubwa 20 vya maji katika maeneo ya Mpera na Kimbiji Wilayani Kigamboni.
Visima hivyo vinavyochimbwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Magufuli kama njia mbadala ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama na kutimiza Sera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kutua ndoo wakina mama wa Tanzania.
Katika ukaguzi huo Mhandisi Alchard Mutalemwa (Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka- DAWASA) alitoa taarifa ya mradi huo wa uchimbaji wa visima 20 (unaogharimu zaidi ya Sh. Bilioni 370 za kitanzania) ambao umekamilika kwa asilimia kubwa na tayari uchimbaji wa visima 18 umekamilika na utazalisha zaidi ya Lita Milioni 260 za maji kwa siku, huku ikimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhandisi Mutalemwa pia alitoa shukrani kwa Mhe. Paul C. Makonda kwa jitihada zake za kutatua kero ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Mkoa wa Dar es Salaam na kumweleza kuwa ahadi yake aliyoitoa wakati wa ziara ya DAR MPYA mwishoni mwaka jana ya uchimbaji wa visima 10 katika majimbo ya Kibamba na Ubungo imezaa matunda ambapo katika majimbo ya Ubungo visima vitano (5) vitachimbwa na jimbo la Kibamba visima vitano (5) ili kupunguza kero kwa wakazi wa majimbo hayo na kuelezea kuwa kukerwa kwake na matatizo ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo kumesababisha kuchukua hatua hiyo.
Uchimbaji huo utaanza karibuni na tayari mkandarasi amepatikana na kazi itaanza mara moja.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda alihoji upatikanaji wa fedha za usambazwaji wa maji yatakayopatikana katika mradi huo wa visima 20 (Mpera, Kimbiji) na kupewa ahadi na Ndg. James Doto Katibu Mkuu wa Fedha aliyeongea nae kwa njia ya simu ya kuwa kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji itapeleka ombi la kupatiwa kiasi cha fedha kilichotengwa na bajeti ya Serikali 2016-2017 (Bilioni 44 za miradii ya maji Dar es Salaam) basi fedha hizo zitapatikana na kusaidia usambazaji wa miundombinu ya maji ikiwemo mradi wa visima 20 (Mpera – Kimbiji).
Mradi wa visima 20 (Mpera – Kimbiji) utasaidia usambazwaji wa maji kwa Wilaya tatu za Temeke, Ilala, na Kigamboni na kumaliza kwa asilimia kubwa tatizo la maji Mkoa wa Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa