Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge amefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali iliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 5 Agosti , 2020.
Awali alianza kutembelea mradi wa machinjio ya kisasa iliyopo Vingunguti katika Manispaa ya Ilala ambako alishuhudia ujenzi unavyoendelea wa machinjio hiyo ulioenda sambamba na uwepo wa vifaa vya kisasa ambavyo vitafungwa kwa ajili ya kutekeleza zoezi zima la uchinjaji wa nyama ili kuwapatia huduma bora wananchi.
Akiwa katika machinjio hiyo alipokea taarifa ya ujenzi huo unavyoendelea na kupongeza zoezi zima linavyoendelea na kueleza kuwa tarehe 30 Septemba,2020 machinjio hiyo iwe imekamilika.
Mhe. Mkuu wa Mkoa Abubakar aliomba wananchi kusaidiwa ili kujua masoko ya kuuzia nyama zao sambamba na uwepo wa huduma zote za msingi kama katika eneo hilo kama vile maji, umeme na barabara nzuri.
Baada ya kutoka katika machinjio ya kisasa ya Vingunguti Mkuu wa Mkoa alielekea katika Ujenzi wa soko la Kisutu ambapo alikagua mradi huo na kupokea taarifa kutoka kwa msimamizi wa mradi huo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa Abubakar alisema haridhishwi na hali ya ujenzi wa soko la Kisutu kwani mradi huo ulipangwa kukamilika Agosti 24,2020 lakini mpaka sasa umekamilika kwa asilimia sitini tu hivyo alitoa miezi miwili tu kwa Mkandarasi kumaliza mradi huo badala ya miezi sita aliyoomba kuongezewa mkandarasi huyo.
Baada ya hapo msafara wa Mhe. Mkuu wa Mkoa ulielekea katika jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ambapo hapo alipokea taarifa kutoka kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya wa Manispaa hiyo ambapo alieleza kuwa utekelezwaji wa mradi huo umekua ukisua sua kwani mpaka sasa TBA ambao ndio wajenzi wa jengo hilo mkataba wao uliisha tangu tarehe 22 Juni,2020 na ujenzi umefikia asilimia sabini na tano tu.
Alieleza kuwa, watumishi wa manispaa hiyo wamekuwa wakifanya kazi kwa tabu sana kwani wako katika maeneo mbalimbali sambamba na Manispaa hiyo kuingia hasara ya kulipa pango katika maeneo ambayo watumishi hao wamepanga.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe. Mkuu wa Mkoa Abubakar alimpatia mkandarasi wa mradi huo Wiki sita tu ili akamilishe mradi huo. Alimtaka mkandarasi wa mradi huo kuweka wafanyakazi wa kutosha sambamba na kufanya kazi usiku na mchana.
Ziara ya Mhe. Mkuu wa Mkoa Abubakar iliishia katika mradi wa stendi ya Mbezi luis ambapo alitembelea na kujionea hali halisi ya mradi huo kisha kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam ambapo alimpongeza Mkurugenzi huyo na Timu yake kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa mradi huo mpaka kufikia hatua iliyopo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa Abubakar alimtaka Mkurugenzi wa Jiji kukamilisha mradi huo ndani ya wakati uliopangwa na kushauri kuwa mradi huo unapokamilika watu wa kuingia wawe wameshapatikana sambamba na kuwepo kwa utaratibu mzuri wa uendeshaji wa mradi huo mkubwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa